Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha kuwepo kwa mvua kubwa kwa siku nne mfululizo kuanzia leo Alhamisi katika baadhi ya maeneo kwenye mikoa 13 ikiwamo visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa ya TMA imesema, mvua hizo zitanyesha hadi Jumapili zikisababisha mafuriko na kuathiri shughuli za kiuchumi kwenye baadhi ya maeneo, huku ikitaka mamlaka na wananchi kuchukua tahadhari.
Maeneo ambayo yametajwa na TMA kuwa na mvua kubwa leo Ahamisi ni mikoa ya Tanga, Morogoro, Pwani ikijumuisha pia kisiwa cha Mafia, Mkoa wa Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kesho Ijumaa, maeneo hayo isipokuwa Morogoro yameripotiwa kuendelea kupata mvua kubwa sanjari na mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Jumamosi na Jumapili, mikoa hiyo itaendelea kuwa na kiwango kikubwa cha mvua sanjari na ue wa Kigoma.
Julai mwaka huu, TMA ilitahadharisha kuwepo kwa mvua za El-Nino kipindi cha msimu wa mvua za vuli ilichosema kitaanza Oktoba hadi Desemba.
Katika taarifa ya mwanzoni mwa Oktoba iliyotolewa na Meneja wa Utabiri wa Mamlaka hiyo, Dk Mafuru Kantamla ilibainisha kwamba El-Nino haitaathiri wakazi wa mikoa yenye Bahari ya Hindi pekee, itasambaa hadi maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini na ukanda wa Pwani.