Tabora. Jeshi la Polisi mkoa hapa limemkamata Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Athumani Msabila na kumhifadhi mahabusu ya kituo cha polisi cha wilaya hiyo.
Mkurugenzi huyo amekamatwa Novemba 5, 2023 mchana baada ya kurejea kutoka mkoani Dodoma alikokwenda kikazi.
Kukamatwa kwa Msabila kumekuja siku mbili baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kumsimamisha kazi Novemba 4, 2023.
Mchengerwa alitoa tamko la kumfukuza kazi Msabila akiwa bungeni jijni Dodoma wakati uchangiaji wa hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC).
Awali, Msabila alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma Ujiji kabla ya kuhamishiwa Igunga.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 6, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Richard Abwao amethibitisha kukamatwa kwa Mkurugenzi huyo.
”Ni kweli Mkurugenzi huyo tunamshikilia akisubiriwa kupelekwa mkoani Kigoma alikotokea kwani ndiko ana kesi.” amesema
Hata hivyo, Abwao hakutaja tuhuma ya kesi inayomkabili Mkurugenzi huyo akiwa katika mojawapo ya halmashauri za mkoa wa Kigoma.