Namungo FC ilizinduka katika mchezo uliopita dhidi ya Azam FC na kufanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-1 mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Simba SC baada ya mchezo wa jana Jumapili (Novemba 05) dhidi ya watani zao, Young Africans itaikaribisha Namungo FC kwenye Uwanja wa Mkapa, Novemba 9, mwaka huu.
Massawe amesema wanatambua Simba SC ni timu kubwa na wanauheshimu ukubwa wao lakini soka lina matokeo ya aina tatu, hivyo wako tayari kuhakikisha wanapambana ili kuondoka na alama tatu.
“Kila mchezaji anafahamu kucheza na Simba SC au Young Africans ni timu za namna gani lakini ni lazima tucheze maana wote tunahitaji matokeo mazuri, na dakika 90 zitaamua,” amesema.
Katika michezo Kuhusu timu yao kutofanya vizuri mechi zilizopita alisema, ni upepo mbaya uliwakumba na wamebaini makosa yao ambayo wanaendelea kuyarekebisha.
“Ligi ni ngumu sana na ina ushindani ni mkali kila timu inapambana kupata matokeo mazuri sehemu yoyote ile, unaweza kufungwa nyumbani ukashinda ugenini ndio soka,” amesema.
Katika michezo minane ambayo Namungo FC imecheza imeshinda mmoja tu, ikipata sare nne na kupoteza mitatu ikiwa na alama saba kibindoni ikishika nafasi ya 12 huku Simba SC ikiwa na alama 18 ikiwa nafasi ya pili baada michezo saba iliyocheza ikiwa imepoteza mmoja.
Simba SC itaingia Uwanja kuikabili Namungo FC huku ikiwa na hasira za kupoteza mchezo dhidi ya Young Africans kwa idadi kubwa ya mabao 5-1.