Pacome Afunguka Utatu wao Yanga 'Lazima Tutoe Mfungaji Bora Msimu Huu'

 

Pacome Afunguka Utatu wao Yanga 'Lazima Tutoe Mfungaji Bora Msimu Huu'

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua amesema kuna sapraizi inakuja msimu huu. Anaamini utatu walioutengeneza utatoa mfungaji bora wa wa Ligi Kuu Bara.


Utatu huo ambao umepewa jina la MAP ukiunda majina ya Maxi Nzengeli, Aziz Ki na Pacome ambao kwenye kikosi cha Yanga wamehusikana mabao 18 kati ya 21 yaliyofungwa. Aziz na Maxi wana saba, huku Pacome akiwa nayo manne.


Akizungumza na Mwanaspoti, Pacome alisema eneo la ushambuliaji la Yanga lina wachezaji wengi wazuri ambao wana jicho la kuona goli, lakini kwenye utatu waliounda anaona mmoja akiibuka mfungaji bora wa ligi kulingana na namna walivyo na ubora.


“Ujio wangu Yanga sikutarajia kama nitakutana na wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa ambao ndani ya muda mfupi tumeelewana na kuisaidia timu kuwa na muunganiko wenye tija ndani ya muda mfupi.


“Ki na Maxi ni wachezaji wa daraja la juu. Siwezi kumuelezea mmoja mmoja sifa zao, kubwa ninaloweza kusema nafurahi kufanya kazi na watu wenye uwezo mkubwa kucheza na kuona goli. Ni wazi kuwa msimu huu Yanga itatoa mfungaji bora katika eneo nalocheza,” alisema Pacome


Pacome alisema ubora wa Yanga eneo hilo unachangiwa na maelewano baina yao na uwezo mkubwa wa mpira wanaocheza kutokana na vipaji na sio mpira wa kufundishwa kwenye uwanja wa mazoezi, na ana furahia kazi anayoifanya kuwa rahisi baada ya kukutana na mafundi wenzake wawili.


“Sina kazi ngumu ya kufanya uwanjani. Narahisishiwa mambo mengi. Nacheza kwa kujiamini nikiwa pamoja na wachezaji hao. Naamini hata wao wanacheza bila wasiwasi kwani tumekuwa tukicheza kwa kuzungumza zaidi nani afanye nini kwa wakati gani hiyo inaweza kuwa siri kubwa ya mafanikio yetu licha ya vipaji tulivyonavyo,” alisema na kuongeza:


“Ni mapema sana kuzungumzia mchezaji gani muhimu zaidi kikosini. Kila mmoja ana umuhimu kulingana na nafasi. Tumekuwa bora, tumecheza mechi tisa tukipoteza mchezo mmoja, huu ni mwanzo mzuri na ukiangalia mimi ni msimu wangu wa kwanza kucheza ligi ya Tanzania, lakini nimeweza kuendana na uchezaji wa wenzangu, hili najivunia.”


Akizungumzia penalti aliyoipiga dhidi ya Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 5-1, alisema: “Sikuandaliwa kupiga mkwaju wa penalti niliambiwa eneo la tukio na haikuwa rahisi kwani licha ya kuwa mbele kwa mabao manne niliamini mashabiki walihitaji furaha zaidi na ndio maana baada ya kupiga na kukwamisha mpira nyavuni nilipata furaha ya kushangilia sana.


Yanga inajiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad utakaopigwa Novemba 24 nchini Algeria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad