Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi Paul Makonda amesema kuhusu tuhuma za Mbunge wa Babati Mjini mkoani Manyara Pauline Gekul, CCM inazo kanuni na taratibu na suala hilo litakapofika katika ngazi ya Taifa watatoa taarifa ya nini kimetokea.
Makonda ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam wakati akijibu swali la mmoja wa Waandishi wa Habari aliyetaka kujua kuhusu hatua za Chama hicho juu ya tuhuma zinazomkabili Mbunge huyo “Kanuni zipo, tuna Mamlaka za nidhamu lakini pia tuna Watu wa maadili kwahiyo kama kuna jambo litakalobainika basi taratibu zitafuata mkondo wake”
Mbunge Gekul anakabiliwa na tuhuma za kumfanyia ukatili Mfanyakazi wake aitwaye Hashimu Ally na mwenzake ambapo tayari Jeshi la Polisi limethibitisha kumuhoji Mbunge huyo na Watu wengine wawili na kusisitiza kuwa hakuna Mtu yeyote aliye juu ya sheria huku RPC George Katabazi akisisitiza kuwa Jeshi hilo litasimamia upatikanaji wa haki kwa mujibu wa sheria.