Paul Makonda Atetea Uteuzi Wake CCM


Paul Makonda Atetea Uteuzi Wake CCM


Sengerema. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema licha ya kelele nyingi kuhusu yeye, lakini Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alisimama imara na kupeleka jina lake katika kikao cha Halmashauri ya CCM kwa uteuzi.

Alisema msimamo huo wa mwenyekiti ulitokana na kuwa na imani naye katika utendaji usio na shaka na kuwa kwake mkweli, hivyo akampa nafasi kubwa yenye heshima ya kukisemea chama hicho.

Makonda alieleza hayo jana wilayani Sengerema, mkoani Mwanza wakati akizungumza na wakazi wa wilaya hiyo kwenye ziara katika Kanda ya Ziwa.

"Hizi ndizo sababu zilizomfanya mwenyekiti kulipeleka jina langu katika kamati kuu hadi Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), licha ya makelele yote, aliziba masikio na kusema Makonda najua ni mkweli na mwaminifu, akisema yupo na wewe basi yupo na wewe kweli, kama hakutaki hakutaki, basi," alisema.


NEC ya CCM ilithibitisha uteuzi wa Makonda Oktoba 22 mwaka huu na kuacha vumbi la mjadala maeneo mbalimbali nchini na hata ndani ya chama hicho.

Wapo waliopongeza na wengine wakikosoa na kuhoji hatua ya kumrudisha kiongozi huyo kwenye reli katika nafasi nyeti ya CCM, licha ya shutuma na tuhuma mbalimbali alizokuwa anatupiwa.

Akijenga hoja hiyo kueleza hayo, Makonda alidai kumekuwa na unafiki wa kujipendekeza kwa baadhi ya viongozi kuwakana watu wema, hasa waliofariki dunia, akiwemo John Magufuli na kujiunganisha na mtu mwenye nafasi ili kuonekana wema.


"Niwaambieni wananchi wa Mwanza, nafahamu mimi ni zao la Magufuli katika safari yangu ya siasa, lakini nafahamu mchango wa Mama Samia katika safari yangu ya kisiasa. Siwezi kufika mahala na kujifaragua na kusahau, mimi ni mkweli na ukweli utabaki kuwa ukweli," alisema Makonda.

Alisema uzuri wenyewe Rais Samia anawajua na kuwatazama, kuwajua waliokuwa na uhusiano na Hayati Magufuli, lakini leo wanavyomkana na kumgeuka anawaangalia viongozi wa namna hiyo.

"Leo (Samia) anapata picha, ipo siku hawa watu watamkana yeye akiwa pembeni. Kwa hiyo wengine Rais Samia anao lakini anawaangalia tu, anajua ipo siku...Makonda hayupo katika hilo kundi kwa sababu ananijua mimi ni mkweli, anajua nikitamka kitu nimetamka, ndiyo maana Rais Samia aliniteua kushika nafasi hii," alisema Makonda, aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

Kuhusu nafasi hiyo, Makonda alisema ni ya wananchi wa Kanda ya Ziwa, ikiwemo Mwanza, hivyo ameamua kufanya ziara ya kutoa shukrani kwa wananchi wa mikoa hiyo, akianzia Kagera.


"Mlikuwa mnaniulizia mbona kijana wenu haonekani, imekuwaje mbona umri mdogo na ana uwezo wa kutoa mchango, sasa maneno yenu na mate ya wazee wangu yamefanya Mungu kusikia na kuweka moyo wa upendo na ujasiri kwa Rais Samia kulibeba jina langu. Mjue cheo hiki tumepewa wananchi wa Kanda ya Ziwa yote, hasa Mwanza," alisema Makonda.

Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu alisema: "Makonda ameamua kuingia Sengerema kwa tipa la mchanga, hii inaonyesha namna anavyojua shida za wananchi.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad