Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amewaomba wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kumuombea awe mwaminifu, mwenye busara na sauti ya wanyonge katika utekelezaji wa majukumu yake.
Makonda aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliteuliwa kushika nafasi hiyo na Halmashauri Kuu ya CCM iliyokutana Oktoba 22, 2023 jijini Dodoma, akichukua nafasi ya Sophia Mjema aliyeteuliwa kuwa mshauri wa rais katika masuala ya wanawake, watoto na makundi maalumu.
"Mniombee nisiingie katika hili jopo nikabweteka, nikasahau...nyinyi ndugu zangu maisha yangu ndio maisha yenu. Mkienda kanisani na msikitini mwambie Mungu tumemtuma Makonda mkumbuke na umpe hekima, busara na msaidizi mzuri wa Rais Samia (Suluhu Hassan)," amesema Makonda.
Ameeleza hayo leo Jumamosi Novemba 11, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Katoro wilayani Geita aliposimama kuwasilimia akielekea Geita mjini.
Tangu kuanza kwa ziara yake, Novemba 9, 2013, Makonda amekuwa akisimama na kusikiliza kero au kupokea taarifa za maeneo husika na kuwapigia simu mawaziri ili kusaka ufumbuzi au majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi.
Makonda amesema uzuri wenyewe ana baraka za bosi wake, Daniel Chongolo (katibu mkuu wa CCM), aliyemtaka kuchapa kazi bila hofu wala uoga wowote au kutishwa.
Katika hatua nyingine, Makonda amewaaambia WanaCCM wa mikoa ya kanda ya ziwa kuwa wana deni kubwa la kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anapata kura za kutosha zitakazomwezesha kuwa Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Amewataka wananchi wa mikoa ya Kagera, Tabora, Mara, Shinyanga, Geita, Mwanza na Simiyu kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada anazozofanya za kuhakikisha Serikali inawapelekea maendeleo kwenye sekta mbalimbali za afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Katika maelezo yake, Makonda amesema Serikali inajitahidi kuteleleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutatua changamoto za Watanzania wakiwemo wa kanda ya ziwa hivyo, aliwataka kutomuangusha Rais Samia katika mchakato wa uchaguzi ujao.
"Nimepewa hii nafasi (uenezi na itikadi), sio kwamba nipo peke yangu,bali nimepata nikiaminiwa kuwa nipo na nyinyi (wananchi).Ombi langu wananchi wa kanda ya ziwa haya mapokezi mlionipa ni ishara tosha Rais Samia hakukosea kunipa nafasi hii hivyo tusimuangushe.
"Kwa tasfiri nyingine tunalo deni la kuhakikisha tunaifanya vema kazi ya CCM, ukiwa na ndugu yako ni rahisi mambo kwenda sasa mimi ndugu yenu nimo.Nina deni kubwa kwa Rais Samia la kuhakikisha ninamlinda na kumtetea na wananchi wa kanda ya ziwa tuna jukumu la kumuombea," amesema Makonda.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge na wananchi wa mkoa wa Geita, Mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani amesema pamoja na Serikali kutekeleza masuala mbalimbali lakini Katoro bado kuna shida ya maji, akimuomba Makonda kuwasaidia.
"Tumepata fedha nyingi lakinj yapo mambo mawili ya kukueleza ili ukipata nafasi uyasukume, hapa kuna shida ya kidogo ya maji. Ukipata nafasi tusukumie kwa watendaji waingie site ili maji yaanze kumiminika katika mitaa ya Katoro na Buseresere," amesema Dk Kalemani.
Kama ilivyo kawaida au staili yake ya mzege halilali, Makonda alimpigia Aweso alisema moja changamoto ya Katoro na Buseresere ni upatikanaji wa maji safi na salama, lakini aliwahakikishia Serikali inafanya kazi na kuna mradi wa Sh 6 bilioni ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 92.
"Naomba unipe wiki tatu wana Katoro na Buseresere watakunywa maji safi na salama yenye kutosheleza," amesema Aweso kwa simu huku Makonda akitaka kuwa na uhakika na ahadi hiyo, lakini waziri huyo alisisitiza kuwa watapata maji kwa muda huo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema Rais Samia alipita eneo hilo mwaka jana katika ziara ya mkoa huo na moja kero iliyotolewa na wananchi ni taa za barabarani, lakini hivi sasa zimeshawekwa kwa kilomita mbili.
"Lakini eneo jingine lililoombwa na wananchi ni uboreshaji wa barabara za mtaani, ninachotaka kuwaahidi wananchi ahadi ya Rais Samia itatekelezwa na wataalamu wameshaelekeza kuanza upembuzi yakinifu," amesema Shigela.