Polisi watatu mbaroni madai unyang’anyi, wizi wa mil. 90/-




MAOFISA watatu wa Jeshi la Polisi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za unyang'anyi wa kutumia silaha na kuiba Sh. milioni 90.

Washtakiwa hao ni Koplo Ramadhani (42) maarufu Rasta, Koplo Majid Abdallah (35) na Koplo Stella Mashaka (40).

Wakili wa Serikali, Neema Moshi, aliwasomea washtakiwa hao shtaka moja la unyang'anyi linalowakabili, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi.

Alidai washtakiwa kwa pamoja Agosti 28, mwaka huu, maeneo ya Kurasini, jirani na Ofisi ya Uhamiaji, wilayani Temeke, waliiba Sh. milioni 90.

Wakili Neema alidai washtakiwa kabla na baada ya kuiba fedha hizo, walimtishia kwa bunduki Grace Matage kwa nia ya kujipatia fedha hizo.


Baada ya kusomewa mashtaka washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Upande wa washtakiwa haukuwa na pingamizi, mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Novemba 13, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Msumi aliamuru washtakiwa warudishwe rumande hadi tarehe hiyo kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad