Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuzima tukio la ujambazi uliopangwa kufanyika katika eneo la Kampuni ya Kijiji Park, iliyoko Kibada Kigamboni, wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana tarehe 17 Novemba 2023, Kamanda wa kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, amedai kundi la watu sita wanaodaiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za jadi, walivamia eneo hilo usiku wa jana Alhamisi, kwa lengo la kutaka kuiba mafuta yaliyohifadhiwa chini ya ardhi.
Kamanda Muliro amedai kuwa, kundi hilo baada ya kuingia ndani ya eneo wakiwa na gari aina ya fuso walianza kumfunga kamba mlinzi kisha kuanza kuiba mafuta. Lakini kabla hawajamaliza polisi walifika na kuanza kuwadhibiti.
“Jeshi la Polisi baadae lilipata taarifa toka kwa watu wema na kufika haraka eneo la tukio.Alikutwa mlinzi akiwa kwenye hali mbaya akaokolewa na baadae wahalifu hao walijaribu kuwashambulia askari ambao walijihami haraka na kuwajeruhi wawili miongoni mwao kwa risasi,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza:
“Watuhumiwa hao walipelekwa hospitali wakiwa na hali mbaya na majina yao hayajafahamika. Mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa eneo la tukio ni Nelson Mbewe (49), mkazi wa Ubungo Kibangu na anahojiwa kwa kina juu ya tuhuma hizo za unyang’anyi wa kutumia silaha kwa kuvamia eneo hilo. Wahalifu wengine wanaendelea kusakwa na lazima watakamatwa.”