Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewatumia salamu nyingine mashabiki wa Simba akiwaambia ukiacha zawadi ya taji la Ngao ya Jamii alilowaachia kwa heshima, kuna mtu mmoja amewasaidia kumpandisha kuwa staa licha ya kumkuta akidharaulika na kwamba wamtunze klabuni hapo.
Robertinho ameliambia Mwanaspoti kwa simu akiwa kwao Brazili, Simba amewaachia staa mmoja ambaye ni Kibu Denis ambaye kwa ubora aliomuacha nao kama akijiamini kidogo tu hakuna kocha ambaye atakuja na kumweka nje.
Kocha Robertinho aliongeza Kibu ambaye alimkuta Simba hakuwa huyu wa sasa kutokana na kuimarika kwake kwa kujua kucheza kwa nidhamu kubwa wakati wote awapo uwanjani.
Kwenye mechi 19 za Simba chini ya Robertinho, Kibu alianza mechi 11 kwenye kikosi cha kwanza huku nne akikosekana na nne akitokea benchi.
“Simba haikuwa na kombe wakati nakuja hapo kwa miaka miwili, nadhani hiyo ndio zawadi yangu ya kwanza ya kumbukumbu ambayo nimewaachia, lakini nyingine ya pili ni Kibu (Denis). Unakumbuka wakati nafika hata mashabiki walikuwa hawataki kuona nampa nafasi, walimwona kama mchezaji ambaye hafai lakini mimi niliona kitu kwake na baadaye nikamwongezea vitu vidogo,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Kibu kama ataendelea kujiamini atacheza sana Simba hii ni zawadi kubwa kwao wamtunze, ni mchezaji ambaye anaweza sana kucheza kwa nidhamu. Hakuna mwanadamu aliyekamilika, makosa anayo kidogo lakini kama ukimjulia na kumpa maelekezo mazuri kwa utaratibu anaweza kufanya kazi vizuri sana.”
Robertinho aliongeza tayari amemwachia ujumbe Kibu mwenyewe akimtaka kuachana na jinsi mashabiki wanavyomchukulia majukwaani na afanye kazi kwani watanyamaza kupitia kazi yake nzuri.
“Kuna wakati alikuwa akisikiliza makelele ya mashabiki, nikamwambia aachane nayo na hata nilipoondoka nimemwambia ayaache, mashabiki wako hivyo, yeye afanye kazi uwanjani akifunga watanyamaza tu.”