Mahakama ya Rufaa imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake ambao ni Silvester Nyegu na Daniel Mbura baada ya upande wa Jamhuri kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu kuwaachia huru kwenye kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Rufaa hiyo ambayo ilisikilizwa na Majaji watatu wakiongozwa na jaji Jacobos Mwambegele upande wa Jamhuri ulileta hoja tano ikiwemo Mahakama kukosea kuwaachia huru Washtakiwa huku wakitaja sababu upande wa Jamhuri kutokutoa nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso kwa Shahidi wa pili
Akisoma hukumu hiyo Naibu Jaji wa Mahakama ya Rufani Abeesiza Kalegeya amesema Mahakama hiyo imeunga mkono hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akisema Mahakama hiyo imeona hakukuwepo tukio la unyang’angyi wa kutumia silaha badala yake Mjibu rufani wa kwanza Lengai Ole Sabaya alikuwepo katika majukumu ya kufuatilia makosa ya uhujumu uchumi kama ilivyoelezwa na Mashahidi wenyewe wa upande wa mashtaka
Mahakama hiyo ya Rufaa imeeleza zaidi kwamba, Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyomtia hatiani Sabaya na wenzake ilikosea sana kutochambua ushahidi unaoonesha wazi kwamba, haiijawahi kutokea Jambazi amkamate Mtuhumiwa, amnunulie ndizi na baadaye kumpeleka Polisi kama Mashahidi wenyewe walivyoelezwa kutendewa na Sabaya.