SIMBA inaangalia uwezekano wa kumpa mkataba wa kudumu mshambuliaji wake, Jean Baleke, kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao.
Baleke hivi sasa yupo kwa mkopo Simba, akitokea Klabu ya TP Mazembe ya nchini DR Congo ambayo alijiunga nayo katika usajili wa dirisha dogo msimu uliopita.
Mshambuliaji huyo hivi karibuni ilielezwa kuwepo katika mipango ya kutimkia nchini Ufaransa, ambako ilielezwa moja ya klabu kumuhitaji.
Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya uongozi wa Simba, amesema kuwa, mazungumzo ya awali yameanza na TP Mazembe kwa ajili ya kumuachia jumla mshambuliaji huyo.
Bosi huyo alisema mazungumzo yanakwenda vizuri kati ya uongozi wa TP Mazembe, ambayo muda wowote yatafikia muafaka na kupewa mkataba mnono wa miaka miwili wenye gharama kubwa.
Aliongeza kuwa, uongozi huo pia upo katika mipango ya kukisuka kikosi chao, katika dirisha dogo msimu huu, kwa kuingiza wachezaji wenye hadhi ya kuichezea timu hiyo.
“Uongozi upo katika hatua za mwisho za kumpa mkataba wa kudumu Baleke, ambaye mkataba wake wa mkopo kutoka TP Mazembe unaelekea ukingoni.
“Tayari makubaliano yanakaribia kufikia mwishoni, na huenda Baleke akasaini moja kwa moja Simba.
“Baleke atapewa mkataba huo, kutokana na mahitaji ya timu katika kuhakikisha wanakiboresha kikosi katika dirisha dogo la usajili msimu huu,” alisema bosi huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alizungumzia hilo la usajili hivi karibuni kwa kusema: “Tumepanga kukifanyia maboresho kikosi chetu katika dirisha dogo, kila mtu ameona upungufu wa kikosi chetu tangu kuanza kwa msimu huu.”