Simulizi ya majonzi baba wa mtoto aliyefia Israel

Simulizi ya majonzi baba wa mtoto aliyefia Israel


Baada ya kupata taarifa ya vita vya Israel na Palestina Oktoba 7 mwaka huu, baba mzazi wa Clemence Mtenga, Mtanzania aliyefariki dunia nchini Israel amesema siku hiyo alimtafuta kijana wake kwenye simu bila mafanikio.


Akizungumza kwa huzuni, Felix Mtenga, mkazi wa kijiji cha Kirwa wilayani Rombo alisema aliendelea kumtafuta mtoto wake kwa siku nne mfululizo bila kupatikana hewani, hivyo alianza kupata wasiwasi.


“Niliwajulisha dada zake, nikawauliza kama wamewasiliana naye, wakasema hawampati hewani, japo waliniambia ni hali ya mawasiliano, nikawakatalia," alisema.


Haikuwa kitu cha kawaida kwa kijana wake kutopatikana kwa siku zote hizo, kwani anasema kila Jumapili alikuwa akizungumza naye, lakini Jumapili ya Oktoba 8 ikapita bila kuwasiliana.


“Tuliendelea kumtafuta bila mafanikio, mdogo wake alituma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) haikujibiwa, hadi siku tulipopata taarifa kwamba yeye na mwenzake walitekwa na hawapatikani,” alisema mzee huyo kwa masikitiko.


Alisema waliendelea na jitihada za kumtafuta kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Israel, Serikali, watu wa haki za binadamu na wengine.


“Baadaye tuliambiwa vinahitajika vipimo vya vinasaba (DNA), wiki mbili zilizopita vilichukuliwa vipimo tukawa unasubiria majibu, juzi (Alhamisi iliyopita) nilizungumza na balozi ndipo akaniambia baada ya vinasaba kufika kule katika utambuzi ndipo wakagundua Clemence ni marehemu.


“Jana (juzi) mkuu wa wilaya alikuja kuniletea taarifa kuwa kijana wangu hatuko naye tena," alisema mzee huyo, akibainisha pia safari ya kijana wake huyo kwenda Israel ilivyokuwa.


Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro, Agosti alipochaguliwa kwenda Israel kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.


“Alikuja nyumbani kutuaga, alikaa wiki mbili, aliniaga akarudi Morogoro kwa ajili ya kuungana na wenzake ili kwenda Dar es Salaam kuanza safari kwa pamoja nchini Israel.


“Aliondoka asubuhi kwenda Morogoro na alipofika tuliendelea kuwasiliana hata siku alipoondoka Dar es Salaam aliniambia anakwenda kupanda ndege na akaniaga na alipofika alinipigia simu na namba ya Israel kunijulisha wamefika salama na kunipa namba yake ya kule,” alieleza.


Alisema tangu kijana wake amefika nchini humo, walikuwa na tabia ya kuwasiliana kila Jumapili kujuliana hali, hadi Oktoba 7 baada kupata taarifa ya vita hivyo na kumtafuta bila mafanikio hadi alipopelekewa taarifa kwamba amefariki.


“Sina cha kusema kuhusiana na tukio hilo, naamini kilichompata kijana wangu ni ajali kama ajali nyingine, Serikali isikatishwe tamaa na tukio hilo katika kusaidia vijana kwenda kujifunza Israel,” alisema.


Novemba 17, mwaka huu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilithibitisha kupokea taarifa za kifo cha Clemence Mtenga, miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani walipo baada ya kuanza kwa vita hivyo.


Taarifa hiyo iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano ya Serikali cha wizara hiyo, ilieleza Clemence alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania 260 waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.


Katika taarifa hiyo, wizara ilieleza taratibu za kuurejesha mwili wa kijana huyo zinaendelea kwa kuwasiliana na Serikali ya Israel, ili mazishi yafanyike nchini, huku wizara ikiendelea kufuatilia taarifa za kijana mwingine, Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo.


Tangu kuanza kwa vita hivyo, inaelezwa zaidi ya Wapalestina 12,000, Waisrael 1,200 wakijumlishwa na waandishi wa habari 42 wamepoteza maisha.


Waisubiri Serikali Mwenyekiti wa Ukoo, Boniphace Mtenga ambaye pia ni msemaji wa familia hiyo alisema wamefanya mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na wametakiwa kusubiri taratibu za Serikali kurudisha mwili nchini.


“Kwa sasa hatujapanga taratibu za maziko, katibu mkuu alituambia wataendelea na mawasikiano na Balozi nchini Israel na majibu yatapatikana kuanzia Jumatatu, hivyo tunaisubiri Serikali iseme mwili unaletwa lini ndipo tutaendelea na taratibu nyingine na kupanga siku ya kumhifadhi kijana wetu.


“Familia tumepokea kwa masikitiko makubwa sana, maana kijana huyu tulikuwa tunamtegemea tukijua atakapohitimu masomo yake, atakuja kuinua wadogo zake na ndugu zake wengine, hata ukoo tulimtegenea, lakini yale matazamio yetu na baba yake yamekatwa ghafla," alisema na kuongeza;


“Kusomesha mtoto kuanzia shule ya mshingi hadi chuo kikuu si kitu cha mchezo, hivyo shida si kwa Felix peke yake, ni pamoja na ukoo mzima na Taifa nzima. Hatujaweza kumtumia kwa njia moja ama nyingine, kwani ameondoka kabla hatujaonja matunda ya elimu yake," alisema.


Alisema mpaka sasa hawajui alifikwa na umauti kwa namna gani, kama alipigwa risasi au nini kilitokea na kwamba wanasubiri mwili ufike ndipo wajue nini kilitokea na kueleza kwamba wengi wanafikiri vita hivyo haiwahusu kwa kuwa wako mbali, lakini inawakuta kwa namna ya tofauti kama ilivyokuwa kwao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad