SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameagiza wakuu wa shule zilizoko wilayani Tunduma, Mkoa wa Songwe, waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za kuwachezesha wanafunzi nyimbo iliyo kinyume na maadili, wapewe nafasi ya kusikilizwa na kama itabainika tukio hilo lilitokea wakati hawako shuleni, warudishwe kazini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Spika Tulia ametoa agizo hilo leo tarehe 6 Novemba 2023, bungeni jijini Dodoma, akidai kuna taarifa zinazoonesha kwamba, wakuu hao wameadhibiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa, lakini pia wakati tukio hilo linatokea walikuwa nje ya shule.
“Hatua za kinidhamu zina pande mbili, huyu kakosea ana haki ya kusikilizwa, aliyesimamishwa bila kusikilizwa utaratibu ukoje? Kama hakuwepo au alikuwepo tunaweza kuthibitisha tuseme sasa, lakini kama mamlaka ilitoa adhabu bila kujua na kama waliamua wakati hakuwepo shuleni na mamlaka ilichukua hatua bila kuwasikiliza warejeshwe kwenye nafasi zao,” amesema Spika Tulia
Akizungumzia agizo hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, amesema walimu hao wanapaswa kukata rufaa ili tukio hilo liangaliwe upya.
“Hilo suala ni la kinidhamu, kama hawakuwepo wanapaswa kukata rufaa kwa mkurugenzi wa halmashauri. Kama mtu amechukuliwa hatua kinyume na utaratibu kama hakuhusika moja kwa moja anaruhusiwa kukata rufaa. Sisi tulitoa agizo kwa mkurugenzi achukue hatua,” amesema Prof. Mkenda.
Walimu hao walifukuzwa shule baada ya video kusambaa mitandaoni ikionesha wanafunzi wakicheza wimbo wa Honey, ulioimbwa na msanii Zuchu.