Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imesema katika siku za hivi karibuni, hakuna chama chochote cha siasa ambacho kimeomba kibali cha kuingiza ndege nchini hayo yamesemwa leo wakati wa kutolewa kwa ufafanuzi wa habari iliyosambaa kuhusu kibali cha ndege iliyokodiwa na CHADEMA .
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema TCAA imesikitishwa na taarifa zinazochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu mamlaka hiyo kutotoa kibali kwa ndege aina ya helikopta iliyokodiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Amesisitiza kuwa mamlaka inapenda kufafanua kwamba siku za hivi karibuni hakuna chama chochote cha kisiasa kilichoomba kibali cha kuingiza ndege nchini hata hivyo Oktoba 20, 2023 mamlaka ilipokea ombi kutoka kwa wakala wa vibali vya ndege kwa ajili ya kuainisha maeneo ambayo viongozi wa CHADEMA watakuwa wakiruka na kutua katika maeneo yasiyo rasmi lengo la kufanya mikutano ya hadhara .
“Wakala huo alishauriwa kuwasilisha ombi la kibali cha kuingiza ndege nchini kupitia mfumo rasmi ili wataalamu wetu waweze kufanya ukaguzi wa nyaraka na pia kujiridhisha na hali ya maeneo ambayo ndege hiyo ilitarajiwa kutua na kuruka kwa mujibu wa sheria ya usafiri wa Anga, sura ya 80 pamoja na kanuni zake kupitia AIC 07/22 (White 161 07 OCT,doc .No.TCAA /FRM/ANS/AIM/-30.” amesema Mkurugenzi Mkuu.
Pia amesema wakala huyo hajawahi kurudi kwetu tena maombi rasmi kama aliyoelekezwa mpaka siku ya leo tunapotoa ufafanuzi huu kwa Umma na pia mamlaka hiyo imeshauri kwamba waombaji wazingatie sheria na taratibu zilizowekwa na Mamkala ya Usafiri wa Anga.