TETESI: Timu ya Simba Wako Katika Mpango wa Kumwajiri Kocha Nabi Kuwa Kocha Mkuu



SIMBA imeanza msako wa kutafuta kocha kwa kasi wa kumrithi aliyekuwa Kocha Mkuu wa Roberto Oliveira ‘Robertinho.’ Na habari zinashtua mtaa wa pili, yaani kule Jangwani ni kwamba mabosi wa timu hiyo fasta wamemrukia aliyekuwa Kocha wa Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Nasreddine Nabi.

Nabi aliiongoza Yanga kwa zaidi ya miaka miwili akiipa mataji sita yakiwamo mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao za Jamii (mara mbili) na kuifikisha timu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na alilikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya sare ya 2-2 na USM Alger ya Algeria.

Kwa sasa kocha huyo yupo FAR Rabat ya Morocco baada ya dili lake la kutua Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kukwama na taarifa kutoka Ubelgiji ilipo familia yake ni kwamba Simba imefanya mazungumzo ya awali na Nabi ambaye kwa sasa yuko Morocco na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya ‘Botola Pro’.

Nabi ameijulisha familia yake juu ya simu hiyo iliyomshtua akiwaambia amefanya mazungumzo ya awali na wekundu hao ambao waliwahi kufanya makosa ya kumtaka kisha kumuacha. Nabi alitakiwa na Simba awali alipokuwa na Al Merrikh ya Sudan kabla ya kumpotezea kutokana na kutimuliwa na timu hiyo.

Simba baada ya kumpotezea Nabi, ilimchukua Didier Gomes, lakini kwa sasa baada ya kuachana na Robertinho, wamerudi tena kwa kocha huyo Mbeligiji mwenye asili ya Tunisia. Mabosi wa Simba wanaamini kwa hali iliyopo kwenye timu, yeye ndiye kocha mwaafaka kuirudisha kwenye ramani ya kutamba kama ambavyo alivyofanya kwa watani wao Yanga ambao bado wameendelea kuwa juu licha ya Mtunisia kuondoka.

Mwanaspoti limejiridhisha juu ya taarifa hiyo kupitia kwa mtoto wa kocha huyo, Hedi Nabi ambaye alijibu kwa kifupi jana kwa njia ya simu kuwa uamuzi utakuwa kwa baba yake na klabu yake ya FAR Rabat.

“Ni kweli Simba wamemfuata baba, lakini sitaki kuliongelea hilo kwa undani kwa kuwa kwa sasa kocha yupo kwenye mkataba na FAR Rabat ni vyema hili likaheshimika kwanza,” alisema Hedi na kuongeza;

“Kwa sasa sijui kipi kitaendelea sisi kama familia kuna maoni yetu tumempa, lakini naye (Nabi) atapima mwenyewe na jinsi gani Simba inayomtaka itashughulikia mkataba alionao na FAR Rabat.


Nabi akiwa FAR Rabat licha ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini amehakikisha anaendeleza ubabe kwenye mashindano ya ndani akiongoza msimamo wa ligi.

Kwenye mechi nane alizoiongoza Rabat, Kocha Nabi inayomilikiwa na Jeshi la Mfalme kushinda michezo mitano sare mbili na kupoteza moja tu, huku ikikusanya alama 17.

Taarifa kutoka ndani ya Morocco zinasema Nabi hana furaha Rabat baada ya timu hiyo kushindwa kuwasajili mastaa wakubwa baada ya kuwauza mastaa wawili muhimu.


Mmoja kati ya mastaa ambao aliondoka Rabat ni Reda Slim aliyeuzwa Al Ahly ya Misri aliyeifunga Simba bao la kwanza hapa nchini kwenye mchezo wa robo fainali ya African Football League Simba ilipolazimishwa sare ya 2-2 kabla ya kwenda kupata sare ya 1-1 ugenini na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini.

Simba inataka kupata kocha wa haraka kuziba nafasi ya Robertinho ili kuzima vurugu za baadhi ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakali kwa mabosi wa klabu hiyo wakiwashinikiza kuachia ngazi. Kama Nabi atafanikiwa kutua Simba, itakuwa ni muendelezo wa rekodi zake kuruka mtaa kama ambavyo alifanya nchini Sudan alipohama kutoka Al Hilal na kutua Al Merreikh ambao ni watani wa jadi.

Hakuna kiongozi wa Simba aliyepatikana kuthibitisha juu ya tarifa hii, kwani simu zao ziliita bila kupokelewa ikidaiwa walikuwa wanaendelea na kikao kizito kilichoanza juzi kujadili mambo ya klabu hiyo .

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad