Tangu Januari mwaka huu hadi sasa, Staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz ametia mkono tuzo saba za kimataifa, mafanikio hayo yanamfanya kutanua ushindi wake wa tuzo barani Ulaya na ukanda wa Afrika Mashariki.
Utakumbuka Diamond alitoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Kamwambie (2009) chini ya Sharobaro Records kisha kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2010 kama Msanii Bora Chipukizi.
Na tangu wakati huo amekuwa na mwendelezo mzuri kimuziki, ametoa albamu tatu, Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), A Boy From Tandale (2018) pamoja na Extended Playlist (EP) moja, First of All (FOA) (2022).
Ndiye mwanzilishi wa WCB Wasafi iliyotengeneza majina makubwa katika Bongofleva kama Harmonize, Rayvanny, Lava Lava na Zuchu, huku Queen Darleen, Rich Mavoko na Mbosso wakijiunga na lebo hiyo ili kuendeleza vipaji vyao na kuvutia biashara mpya.
ULAYA
Ni wikiendi iliyopita tu Diamond alishinda Tuzo ya MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2023 katika kipengele cha ‘Best African Act’ na kuandika rekodi nyingine katika tuzo hizo ambazo zimekuwepo kwa miaka 28.
Ushindi wa Diamond ni wa kishindo kutokana na aina ya watu aliokuwa anashindana nao ambao ni Burna Boy (Nigeria), Asake (Nigeria), Libianka (Afrika Kusini) na Tyler ICU (Afrika Kusini).
Diamond mwaka uliopita alikosa tuzo hiyo na ushindi ukaenda kwa Burna Boy, ushindi wake kwa mwaka huu umemfanya kuandika rekodi kama msanii wa kwanza wa Afrika kushinda tuzo tatu za MTV EMA.
Tayari Diamond alikuwa na tuzo mbili alizoshinda Oktoba 2015 huko Milan Italia ambapo aliandika rekodi kama msanii wa kwanza kutoka Afrika kushinda tuzo mbili za MTV EMA katika vipengele viwili kwa msimu mmoja.
Ikumbukwe Diamond alishinda katika vipengele vya ‘Best African Act’ na ‘Best Worldwide Act/ India’ ambacho Miss World 2000 na Staa wa filamu India, Priyanka Chopra naye alikuwa anawania.
Tuzo za MTV EMA zilianza kutolewa Novemba 24, 1994 katika Ukumbi wa Brandenburg Gate huko Berlin, Ujerumani, na kila mwaka hafla hiyo kutangazwa mubashara na MTV Europe, Channel 5 na vituo vingi vya kimataifa vya MTV.
Chini ya Paramount International Networks, lengo la tuzo hizo ni kuwatunza wasanii na muziki katika utamaduni wa Pop, tangu mwaka 2007, mashabiki wamekuwa wakiwapigia kura washiriki kupitia tovuti ya MTV EMA.
AFRIKA MASHARIKI
Kati ya tuzo saba za kimataifa alizoshinda Diamond kwa mwaka huu pekee, vipengele vitano vinamtaja kama Msanii Bora Afrika Mashariki, hakuna msanii mwingine aliyeweza kufanya hivyo, kwa hiyo tunaweza kusema ubabe wake umekita ukanda huo.Agosti 2023, Diamond alishinda tuzo za East Africa Arts Entertainment Awards (EAEA) kama Msanii Bora wa Mwaka baada ya kuwabwaga Alikiba, Eddy Kenzo, Fally Ipupa, Innoss’B, Koffi Olomide na Sauti Sol.
Akashinda tena kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki, washindani wake walikuwa ni Alikiba, Bruce Melodie, Khaligraph Jones, Eddy Kenzo, Harmonize na Rayvanny.
Vilevile alishinda kipengele cha Chaguo la Watu Wimbo Bora wa Bongofleva (Yatapita), nyimbo nyingine zilizokuwa katika kinyanganyiro hicho ni Naogopa (Marioo & Harmonize), Mahaba (Alikiba) na Utaniua (Zuchu).
Tuzo za EAEA ni kwa ajili ya kuwatunza wasanii wanaofanya vizuri katika mataifa ya Burundi, DR Congo, Kenya, Rwanda, Tanzania, Uganda na Sudan Kusini. Wasanii wengine Bongo waliowahi kushinda ni Zuchu, Mwana FA, Nandy, Rayvanny, Rosa Ree, Barnaba, Mbosso n.k.
Septemba 2023 alishinda tuzo za African Muzik Magazine Awards (Afrimma) kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki baada ya kuwashinda Nyashinski, Bien, Lij Michael, Eddy Kenzo, Mbosso, Harmonize, Meddy na Single Dee. Ikumbukwe tuzo za Afrimma zilianzishwa na Mfanyabiashara wa Nigeria, Anderson Obiagwu, kwa mara ya kwanza zilitolewa Julai 2014 huko Texas, Marekani zikiwa na lengo la kusherekea kazi za muziki, vipaji na ubunifu kote Afrika.
Tuzo hizo zina vipengele 28 na hujumuisha aina zote za muziki kutokea Afrika ikiwa ni pamoja na Afrobeats, Afro-Trap, Assiko, Bongofleva, Coupe-decale, Genge, Highlife, Kwaito, Lingala na Soukous.
Septemba 2023, Diamond alishinda tuzo za The Headies zilitolewa huko Georgia, Marekani, alishinda kama Msanii Bora Afrika Mashariki kufuatia kuwabwaga washindani wake ambao ni Zuchu, Rayvanny, Eddy Kenzo na Hewan Gebreworld.
Tuzo za The Headies zilianza kutolea Machi 2006 na Jarida la Hip Hop World la Nigeria ili kutambua mafanikio bora katika tasnia ya muziki ya Nigeria na baadaye Afrika nzima. Zina jumla ya vipengele 25 na hadi sasa Wizkid ndiye msanii waliyeshinda mara nyingi zaidi ambazo ni 20.
Na Oktoba 2023 Diamond akashinda tuzo ya Trace kama Msanii Bora Afrika Mashariki baada ya kuwazidi kete, Bruce Melodie, Zuchu, Khaligraph Jones, Nadia Mukami na Azawi.
Utakumbuka ili kusherehekea miaka 20 ya kukuza na kuunga mkono muziki wa Kiafrika, Trace aliandaa tuzo na tamasha la kwanza ambalo lilifanyika BK Arena Kigali, Rwanda hapo Oktoba 21, 2023. Matukio hayo yalionyeshwa moja kwa moja kwa watazamaji na mashabiki takribani milioni 350 kote ulimwengu kwenye chaneli za Trace katika nchi 180.