Vita ya Mafahali Wawili Wenye Hadhi ya Kimataifa Simba na Yanga Kwa Mkapa Kutawaka Moto

 

Vita ya Mafahali Wawili  Wenye Hadhi ya Kimataifa Simba na Yanga Kwa Mkapa Kutawaka Moto

Vita ya Mafahali Wawili  Wenye Hadhi ya Kimataifa Simba na Yanga Kwa Mkapa Kutawaka Moto

Mafahari wawili hawakai zizi moja.Jumapili hii itashuhudiwa mcehezo wa kukata na shoka wa ‘mahasimu’ wa Dar es Salaam, Simba na Yanga, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara au NBC Premier League.


Mchezo huu unakuja katika mazingira yanayotaka kufanana na mazingira ya mchezo wao wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita ambao ulizikuta timu hizo mbili zikiwa kileleni kwa kulingana pointi huku Simba ikiwa na faida ya mabao. Wakati huo zilikuwa kwenye mashindano ya Afrika.


Safari hii zinakutana Yanga kikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya mabao ya kufunga. Kama ilivyokuwa msimu uliopita, timu hizi ziko kwenye mashindano ya Afrika lakini safari hii ziko kwenye ngazi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika jambo ambalo litaongeza msisimko kwani ni kwa mara ya kwanza zinakutana zote zikiwa katika viwango vya juu kimataifa.


Pambano la ‘derby’ ni mchezo baina ya timu zinazotokea katika eneo moja au nchi moja au katika mashindano yanayozishirikisha timu mbili zenye upinzani mkali. Neno derby lina asili katika mashindano ya farasi wenye upinzani kwenye miaka ya 1870 katika mji wa Derby ulioko Derbyshire, Uingereza. Katika mpira wa miguu timu upinzani huanza kidogokidogo ukichochewa na mambo kadhaa zikiwemo tofauti za kidini, kisiasa, kipato na hata historia na utamaduni.


Wachezaji huja na kuondoka, makocha huja na kuondoka, viongozi huja na kuondoka na mashabiki huja na kuondoka lakini utani kati ya timu hizo hubaki pale pale. Upinzani huu huonekana dhahiri kwenye siku ya mchezo kati ya mahasimu hawa ambapo shughuli zote husimama. Hakuna mchezo wenye maana kwa klabu yoyote zaidi ya mchezo wa watani wa jadi.


Miongoni mwa mapambano yenye umaarufu mkubwa duniani kwa sasa ni pamoja na Hispania, FC Barcelona v Real Madrid (El Clasico), Italia, AC Milan v Inter Milan (Derby della Maoninna), Scotland, Celtic v Rangers (The Old firm), England, Manchester City v Manchester United (Manchester derby), Manchester United vs Liverpool (North West derby), Arsenal v Totenham Hotspurs (North London derby), Everton v Liverpool (Merseyside derby), Misri, Al Ahly v Zamalek (Cairo derby), Agentina, Boca Junior vs River Plate (Superclasico), Ureno, Porto v S.L Benfica (O Classico). Orodha ni ndefu sana


Mtandao wa kimichezo wa Goal.com umetaja pambano la watani wa jadi wakiliita kwa kimombo Dar es Salaam derby au Kariakoo derby kuwa katika nafasi ya tano kwa ukubwa barani Afrika. Mchezo huo wa watani wa jadi unawakimbiza kwa karibu mapambano mengine ya mahasimu katika nchi za Tunisia, Morocco, Afrika ya Kusini na Misri ( pambano la mahasimu la Cairo) lililo kileleni. Uwekezaji mkubwa na kuongezeka kwa Timu ya Azam FC kama moja ya timu tatu zinazowania ubingwa kunaweza kuongeza ladha katika uhasimu wa kimpira huko mbeleni.


Mchezo kati ya Yanga na Simba umekuwa na mvuto wa aina yake. Pamoja na utani huu kuwa na miaka zaidi ya 80 lakini utani umeshamiri zaidi kuanzia miaka ya baada ya uhuru yaani miaka 60 iliyopita. Timu hizi zinatokea mitaa ya Msimbazi (Simba) na Twiga na Jangwani (Yanga) iko Kariakoo.


Pamoja na kuwa na historia iliyoanzia kwenye siasa, pambano hili limeziacha nyuma historia hizi na kuwa utani wa mpira pekee. Hii pengine ndiyo imesababisha pambano hili kuwa la watani zaidi kuliko mahasimu.Haishangazi familia moja wanatoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kushangilia timu tofauti.


Simba na Yanga huchochea mapenzi na maendeleo ya mpira karibu kwa kila kijana. Ni kutokana na pambano hili ndoto za vijana hufikiria siku moja achezee Yanga au Simba. Waswahili wanasema kuwa kwa kawaida mtu hupenda Yanga na Simba kwanza kisha hupenda mpira wa miguu.


Pambano hili linakuwa mubashara kwenye runinga ambako watu kutoka sehemu mbalimbali hulitazama.Ukweli wa kwamba hata Dar es Salaam linakofanyikia bado runinga huwa mubashara majumbani kwa watu, kwenye mahoteli,kumbi nyingi za starehe na hata vibandaumiza. Bado hilo halizuii watu zaidi ya elfu 60 kwenda uwanjani.Siku za nyuma nilitembelea baadhi ya miji mikubwa Ulaya; wao walizima runinga ikiwa timu za mji mmoja zinapambana kwa maana hawakuwa na uhakika wa kupata watu wa kuujaza uwanja ikiwa mchezo ungekuwa mubashara. Kwa pambano la watani wa jadi la Tanzania ni kinyume kabisa. Ni tukio lenye mizizi haswa mioyoni mwa watu.


Naweza kusema kwa sasa mchezo wa watani wa jadi umefikia kiwango ambacho unaweza kuingizwa kwenye kifurushi cha mtalii (tourist package).Mathalani, mtalii anatua Kilimanjaro kuona Mlima Kilimanjaro na mbuga za kaskazini, kisha anaelekea Dar es Salaam kuangalia mchezo wa watani wa jadi na kutoka hapo anaenda kwenye Visiwa vya Mafia, Pemba. Tiketi za mashirika ya ndege hata meli zinaweza kuunganishwa na tiketi ya kuingia uwanjani na hivyo kuongeza wageni na kuitangaza derby ya Dar es Salaam.


Uzoefu wa hapa ndani umeonyesha hizi timu zimekuwa ni kivutio bila kujali zimekutana Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza, Arusha hata Kigoma. Kwa kuupeleka nje ya Dar es Salaam, mchezo huu utakuwa unaongezewa thamani kama chapa na kupata mashabiki wapya.


Pamoja na mapato yanayotokana na viingilio, haki za runinga, mauzo ya jezi na bidhaa nyingine za klabu, mchezo huu huingiza fedha kwenye nyumba za wageni, kumbi za starehe na kadhalika. Pia, siku ya mchezo huu hutoa ajira za moja kwa moja kwa wahudumu wa mchezo na hata wasafirishaji kama bodaboda.


Yanga ni wanafainali ya Kombe la shirikisho la CAF kwa msimu uliopita lakini pia wako miongoni mwa klabu 10 zinazowania kuchukua tuzo ya klabu ya mwaka 2023 ya Afrika.


Simba ni wanarobo ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia wametolewa katika ngazi hiyo katika ligi ya mpira ya Afrika (African Football League) bila kupoteza mchezo mmoja katika muda wa kawaida wa mikondo miwili waliyocheza na mabingwa wa Afrika Al Ahly.


Sasa wanakutana kwenye ligi ya ndani,lakini kuna uwezekano pia wakakutana kimataifa hata kwenye Ligi ya Mabingwa wa Afrika kama ambavyo tuliwahi kuwaona zaidi ya mara moja wakipambana kwenye fainali za klabu bingwa ya Afrika Mashariki na kati visiwani Zanzibar.Kiwango cha sasa cha klabu hizi kinalifanya pambano hili kuwa la hadhi ya kimataifa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad