Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha tope lote ambalo lipo chini ya daraja lililipo katika eneo la Jangwani linazibuliwa ili maji yaweze kupita badala ya kupindukia barabarani na kupelekea eneo hilo kutopitika ambapo amemuambia Meneja huyo kuwa hicho ni kipimo chake kama anatosha kubaki kwenye nafasi yake ama laah!.
Akiongea leo November 13,2023 baada ya kukagua eneo la Jangwani Jijini Dar es salaam, Bashungwa amesema “Nimemuelekeza Meneja wa TANROADS ambaye ameripoti hapa hana hata mwezi nimemwambia kipimo chake kama anatosha ni kuhakikisha tope chini ya daraja hili linazibuliwa ili maji yanapokuja kabla hayajapindukia barabarani, tope liwe limeondolewa maji yapite, labda yawe mengi sana ndio maji yanaweza kufunika juu ya daraja”
“Watanzania waiamini Serikali ina mipango ya muda mrefu ambayo ni ujenzi wa daraja jipya na mipango ya muda mfupi ikiwemo ya kuondoa tope na kusafisha mifereji, niipongeze Mamlaka ya hali ya hewa ilitoa tahadhari mapema lakini mabadiliko ya tabianchi hakuna anayejua kesho yatakuja kwa njia zipi, tunawaahidi Watanzania tutaendelea kujipanga kama Serikali kujua tunakabiliana nayo vipi”
“Tumekuja hapa tumeona sehemu ya changamoto ni takataka kuziba chini ya daraja na wote Mimi na Waziri Mchengerwa tunawaelekeza Ma-RC na Ma- DC maeneo yote kusimamia na kutoa elimu kwa Watanzania kuzingatia usafi, ukiwa kwenye basi au chombo chochote cha usafiri au unatembea kwa miguu ukinywa maji ukamailiza sio ustaarabu kutupa tu chupa, inazalisha takataka ambazo zinaziba mifereji na madaraja”