Kipa wa Manchester United, Andre Onana amekiri kiwango chake kimeshuka tangu alipotua Old Trafford, lakini amewaambia mashabiki "msihofu sana, mambo yatakuwa sawa."
Kipa huyo Mcamerooni, mwenye umri wa miaka 27, alitua Man United akitokea Inter Milan wakati wa dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya, kama chaguo la kwanza baada ya David de Gea kuruhusiwa kuondoka bure kwenye kikosi hicho.
Onana amekutana na wakati mgumu, akiruhusu mabao 39 katika mechi 25 alizochezea timu hiyo msimu huu, ikiwamo mabao 15 katika mechi sita tu za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya kusemwa sana kuhusu kiwango chake, Onana aliwajibu wanaomkosoa kwa kusema "kipa bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita ghafla tu amekuwa wa hovyo duniani.
"Kama nitazungumzia msimu wangu hadi sasa hapa Man United, sifurahii kwa sababu ningeweza kufanya vizuri zaidi, najua naweza kufanya vizuri zaidi ya hiki kinachotokea sasa.
"Kila kitu ni cha kupita. Najua nitakuwa sawa. Kama sio leo, itakuwa kesho, kama si kesho basi itakuwa siku inayofuata baada ya kesho."
Onana alifikisha mechi yake ya sita bila ya kuruhusu bao kwenye Ligi Kuu England msimu huu, wakati timu yake ya Man United ilipokwenda kumenyana na Liverpool uwanjani Anfield, Jumapili iliyopita na kutoka sare ya bila kufungana.
Onana aliisaidia Inter Milan kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, ambapo kwa msimu huo kati ya mechi 41 alizocheza kwenye michuano yote, 19 zilimalizika bila ya kuruhusu bao.