Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema kutoonekana hadharani kwa kipindi cha mwezi mmoja, kulitokana na kuwa na shughuli na kazi maalumu nje ya nchi.
Dk Mpango ameyasema hayo leo Jumapili, Desemba 10, 2023 alipoonekana kwa mara ya kwanza kushiriki misa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, lililopo Kiwanja cha Ndege mjini Dodoma.
“Mkae na amani, niko salama nimekwenda nje kufanya shughuli maalumu kwa takribani mwezi mmoja, sijapungua hata kidogo,” amesema alipopata nafasi baada ya kumalizika kwa hiyo, akiwataka Watanzania kutumia vema mitandao ya kijamii.
“Asanteni sana kwa kuniombea, yamesemwa mengi, si ndiyo? Na wengine wamesema mimi ni mzuka sasa wale mnaokumbuka mnaosoma biblia, Zaburi ya 118 aya ya 17 inasema, ‘Sitakufa, Nifanyeje’.”
Amesema matumizi yasiofaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakiumiza watu wengi, hivyo yampasa kila mmoja kuitumia vema pamoja na kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.
“Baadhi ya mitandao ni mizuri lakini baadhi ya watu wanaitumia visivyo, inaumiza pia watu wengi. Unaona vijukuu vyangu havijaniona mwezi wamenikimbilia kuja kunifuata,” amesema Dk Mpango ambaye katika misa hiyo alikaa na wajukuu zake wawili.
“Wengi wanaumizwa, kwa hiyo tujitahidi sana kutumia mitandao ipasavyo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu, walikuwa wanatuma picha yangu na mshumaa pembeni, wengine wanasema mzee amekata moto, bado kabisa kazi ambayo Mungu alinituma kufanya sijaimaliza.
“Wakati utakapofika nitarejea kwa Mungu wangu, asanteni sana najua mmeniombea, nimewaona masista pale wametoa machozi na mimi nikatoa ya kwangu, basi Mwenyezi Mungu awabariki sana,” amesema Dk Mpango.
Kabla hajazungumza na waumini wa kanisa hilo, alishiriki misa hiyo iliyoongozwa na Padri Dionis Paskal Safari na amewashukuru waumini hao kwa kuendelea kumuombea ili aweze kutekeleza vema majukumu yake.
Nje ya kanisa, Dk Mpango alizungumza na kaka yake, Padri Sebastian Mpango pamoja na Padri Emmanuel Mtambo.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Mpango alionekana kwa mara ya mwisho, Oktoba 31 jijini Dodoma alipomwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa dharura wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao