Hizi Hapa Sababu 5 Kwanini Simon Msuva Anapashwa Kukubali kusaini Yanga



FAILI la mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ambaye kwa sasa yupo nchini baada ya kumalizana na JS Kabylie ya Algeria, limetua kwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye aliwaambia mabosi wa timu hiyo na uhitaji wa mshambuliaji wa kati kama itawezekana katika dirisha hili.

Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa Gamondi amevutiwa na uwezo wa mshambuliaji huyo hivyo kazi imesalia kwa viongozi kumalizana naye kwani walianza mazungumzo naye tangu alipopewa mkono wa kwaheri na JS Kabylie.

Msuva 30, hakuwa na wakati mzuri akiwa na JS Kabylie kwani katika michezo sita aliyoichezea timu hiyo kwenye ‘Ligue Professionnelle 1’ hakufunga wala kutoa asisti hata hivyo mabadiliko ambayo yalifanywa ya benchi la ufundi nayo yametajwa kuwa sehemu ya kushindwa kuonyesha makali yake.

Mabosi wa Yanga wapo kwenye mazungumzo na Msuva ambaye anasubiri muda aripoti kambini kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi ujao huko Ivory Coast.


Japo hii sio mara ya kwanza kwa Msuva kuhusishwa na Yanga hizi ni sababu tano ambazo zinaweza kumfanya mshambuliaji huyo kurejea tena Jangwani ambako alijizolea umaarufu kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

AMEPATA ALICHOTAKA

Licha ya kuwa bado umri unamruhusu kuendelea kucheza soka la ushindani tayari Msuva ametengeneza mkwanja mrefu kitu ambacho alikuwa akihitaji wakati akiondoka Tanzania 2017 alipotimkia Difaa El Jadida ya Morocco.

Msuva yule ambaye alikuwa akiichezea Yanga ni tofauti kabisa na huyu, alitengeneza pesa nyingi akiwa Morocco achana na zile ambazo alipata kama sehemu ya usajili, posho na mshahara, ile kesi yake dhidi ya Wydad Casablanca alitapa zaidi ya dola za Kimarekani laki saba (zaidi ya Sh1.6 bilioni).


Hakuishia hapo, Msuva alipata dili nono la kwenda Saudia ambako alijiunga na Al-Qadsiah kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja huko nako inaelezwa alitengeneza fedha nyingi ambazo ziliendelea kumweka katika nafasi ya miongoni mwa wachezaji matajiri zaidi wa Kitanzania nyuma ya Mbwana Samatta ambaye inaelezwa hakuna hata mwanasoka mmoja anayemfikia hata nusu.

Mara baada ya mkataba wake kumalizika, Msuva akatua zake Algeria ambako nako amevuna mkwanja mara mbili, moja wakati akisajiliwa na pili mkataba wake ulipovunjwa na JS Kabylie siku chache zilizopita.

UKARIBU NA FAMILIA

Hakuna kitu kigumu ambacho kimekuwa kikiwapa wakati mgumu wachezaji wengi wa Kitanzania kama kuwa mbali na familia zao, kuishi sehemu ngeni ambako kila kitu kinakuwa kipya kwao tofauti kabisa na nyumbani.

Kwa zaidi ya miaka mitano ambayo Msuva amekuwa mbali na familia yake anaweza kuona kuwa huu ni wakati sahihi kwa yeye kuwa karibu na familia yake hata kama itakuwa kwa kipindi kifupi huku akiwa na hesabu kubwa wakati wa dirisha lijalo la usajili moja thamani yake inaweza kuwa imepanda, hivyo anaweza kutengeneza mkwanja zaidi.


LIGI YA MABINGWA

Ushiriki wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika inaweza kuwa kigezo cha Msuva kufikiria mara mbilimbili juu ya ofa ambayo Yanga imeweka mezani kwani ligi hiyo anaweza kuitumia kama jukwaa la kuonyesha makali yake.

Wachezaji wengi wakubwa wamekuwa wakishawishika kujiunga na timu fulani kulingana na ukubwa wake na hata ushiriki wake kwenye michuano mikubwa japo muda mwingine mkwanja nao huwa sehemu ya ushawishi ndio maana mastaa mbalimbali wakubwa wamekuwa wakimiminika huko Mashariki ya kati, Saudi Arabia.

MKWANJA

Yanga ile ambayo Msuva alikuwa akiichezea ni tofauti kabisa na hii, kwanini? Hii ina wachezaji ambao wamesajiliwa kwa zaidi ya dola laki moja na nusu (zaidi ya Sh377 milioni) na hata kuwalipa mishahara mikubwa hadi dola 10,000 kwa mwezi (zaidi ya Sh25 milioni) na hata posho zinaweza kumvuta Msuva kurejea Jangwani.

KUKAA BILA TIMU

Kukaa bila timu kwa mchezaji hushusha thamani yake, hivyo Msuva anaweza kuchangamkia dili la kujiunga na Yanga hata kama itakuwa kwa miezi sita ili asikae bila timu maana Januari na Februari atakuwa na majukumu ya kitaifa huko Ivory Coast.


Hivyo, inaweza isiwe rahisi kupata timu ya kuichezea baada ya fainali hizo, kujiunga na Yanga inaweza kuwa moja ya karata yake muhimu huku akiwa na hesabu nyingine maana Msuva bado anajiona kuwa na nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad