Ishu ya staa Mamelodi Simba iko hivi

 


Hii ni ngumu kumeza. Wakati mashabiki wa Simba wakitamba kwamba viongozi wao wanawasajilia mtu wa kazi, Aubrey Maphosa Modiba (28) kutoka klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, imefahamika huo sio mpango wa kocha Abdelhak Benchikha.


Ishu ya Modiba, anayecheza kama kiungo wa kushoto na pia beki wa kushoto, imeshika kasi kwenye mitandao ya kijamii, kwamba viongozi wa Simba wamekwea pipa kwenda kuzungumza na staa huyo anayetajwa ni miongoni mwa Top 10 katika orodha wa wachezaji ghali zaidi kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL).


Ukweli ambao gazeti la Mwananchi limeupata kutoka kwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba (jina tunalo), unaelezwa Benchikha amependekeza majina mawili ya mabeki wa pembeni akitaka mmoja wao ndio asajiliwe kwa ajili ya kuja kusaidiana na nahodha msaidizi wa timu hiyo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ huku akisisitiza hawana uwezo wa kumchukua Modiba kutokana na ukubwa wa gharama zake.


Chanzo hicho cha uhakika kimesema beki wa kwanza ni Ibrahim Imoro (24), raia wa Ghana anayeitumikia klabu ya Al-Hilal ambaye anaweza kucheza nafasi ya Tshabalala na pia kama kiungo wa pembeni ambako kwa Msimbazi anacheza Said Ntibanzokiza ‘Saido’ na Moses Phiri. Vile vile anacheza kiungo wa kati anapocheza Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.


Beki mwingine ni Hernest Briyock Malonga (21), kutoka klabu ya Diables Noirs ya Burundi, huyo ni raia wa Congo.


Hata hivyo, Benchikha ameshawaambia Simba kuwa hataki wachezaji wengi kwenye dirisha dogo bali kazi kubwa itakuwa mwishoni mwa msimu.


Ugumu kwa Modiba


Baada ya kusambaa kwa habari za staa huyo, alitafutwa beki Mtanzania Abdi Banda anayechezea FC Richardsbay FC au Natal Rich Boys ya Afrika Kusini, ambaye alifichua namna mchezaji huyo alivyo ghali huku kwa mujibu wa Transfermarkt, thamani ya Modiba ikitajwa kuwa ni Euro 1.3 milioni (sawa na Sh3.6 bilioni) za Kitanzania.


“Nafahamiana na Modiba, ni miongoni mwa Top 10 ghali hapa Afrika Kusini, ni kijana na panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Mamelodi, aliipa timu yake ubingwa wa African Football League, sasa siwezi kuzungumza zaidi ya hapo, ila hata maisha yake ya nje ni ghali,” alisema.


Ugumu mwingine wa kumsajili mchezaji huyo ambaye mkataba wake unamalizika  Juni 30, 2025, ni vile timu yake inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kanuni za CAF hazitamruhusu kucheza michuano hiyo kama ingetokea Simba ikamsajili hivyo angebaki kucheza ligi ya ndani pekee.


Mjumbe huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba alisema kwasasa ni vigumu kwao kumsajili nyota huyo kutokana na vigezo alivyonavyo ikiwemo pesa.


“Ni ngumu kumchukua mchezaji huyo kwasasa, anacheza michuano ya CAF halafu pesa yake kiukweli sidhani kama tunaimudu, tunahitaji wachezaji ambao tutawatumia kwenye michuano yote huyo haitakuwa rahisi, hata kwa malengo ya baadaye haiwezekani.


“Kuna hao wawili ambao tumepewa majina yao ila tunasubiri kukutana na kocha ili tuyajadili kwa pamoja, hivyo suala la kukamilisha pia bado, na ni mmoja kati ya hao ndio atachukuliwa,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;


“Tunaangalia sehemu mbalimbali, usajili hautakuwa mkubwa sana ila tunahitaji wachezaji bora kwa nafasi ambao zina upungufu.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad