JE, Njia za Kukata Hedhi Kwa Mwanamke ni Salama? Soma Hii

 

Njia za Kukata Hedhi

Dar es Salaam. Umewahi kusikia au kujaribu kunywa dawa kukatisha hedhi? Kama jibu lako ni ndiyo, basi athari zake ni kubwa, ikielezwa kufanya hivyo ni kujipalia makaa.


Madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini, wanasema moja ya athari za kukatisha hedhi kwa njia hiyo ni kuwa na usugu wa dawa mwilini.


Mbali ya hilo, wanaeleza kisayansi hakuna njia ya kukatisha au kuzuia hedhi katika kipindi husika.


Ijapokuwa wapo wanaofanya hivyo wakitumia njia za kienyeji, madaktari wanasema wanachopata ni matokeo kwa nje, lakini ndani ya miili yao uchafu na damu ya hedhi itaendelea kusalia.


Kauli ya madaktari ni majibu kwa Mwananchi ilitaka kufahamu athari ya kitendo hicho kutokana na baadhi ya wanawake na mabinti kueleza kutumia njia za kienyeji na wengine kumeza vidonge kama vile flagyl na asprini kuzuia damu ya hedhi.


Kwa kawaida hedhi huwa kuanzia siku tatu hadi saba, hivyo baadhi huamua kuikatisha, wengine wakipaka limao ukeni wakiamini wanazuia damu ya hedhi.


Siwema Simon, mkazi wa mji wa Morogoro anasema ameshawahi kutumia dawa kuzuia hedhi baada ya kushauriwa na rafiki yake wa kiume.


"Nilikuwa nikiona damu ya hedhi siku ya kwanza tu, nameza flagyl na huwa ikikata," anasema.


Kwa upande wake, Anjelina Jackson ambaye ni mwanafunzi wa sekondari anasema rafiki yake alimshauri atumie limao kukata hedhi.


"Nilitumia nikaamini inakata, lakini nikaanza kupata vitu kama vile malengelenge sehemu za uke. Hivi sasa sithubutu kurudia jambo hilo," anasema Anjelina anayesoma kidato cha tatu katika moja ya sekondari zilizopo mkoani Dar es Salaam.


Anasema alishawishika kufanya hivyo kutokana na kero alizokuwa akipitia shuleni anapokuwa kwenye hedhi.


Kwa upande wake, Hawa Ibrahim, mama wa watoto wawili anasema alikuwa akimeza flagyl kukata hedhi.


"Nilianza nikiwa binti, ijapokuwa sikuwa nafanya hivi mara kwa mara, mbinu hii nilidokezwa na binamu yangu tuliyekuwa tukiishi pamoja,” anasema na kuongeza:


"Yeye alikuwa akifanya hivyo, siku moja akaniomba nimsindike sehemu, nilikuwa kwenye siku zangu nikawa siko huru, akaniletea flagyl nikanywa, nilishangaa damu ya hedhi ilikata hadi mwezi uliofuata.”

Anasema, "Huo ukawa mchezo wangu, baadaye nikavuruga hata ule mzunguko wangu wa hedhi wa kawaida. Kuna wakati napata maumivu makali ya tumbo tofauti na awali."

 


Athari zilizopo


Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Salaamani iliyopo Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, Abdul Mkeyenge anasema kitaalamu vitu hivyo vinavyotumiwa haviwezi kukata hedhi.


"Hata ukichoma sindano bado uchafu utatoka kwani hedhi si damu peke yake," anasema.


Anasema hedhi ipo moja kwa moja kwa kuwa ni mayai ambayo hayajarutubishwa yanayochanganyika na tishu zilizokufa.


"Kama nilivyosema hizo dawa haziwezi kukata hedhi, ukitumia ndimu au limao bado ni uongo haviwezi katisha na ikitokea umetumia kwa nje ikakata kwa ndani zitakuwapo na si vizuri.


"Hedhi ni tendo ambalo ukipata umekamilika na mfumo wako umekamilika. Unapomeza dawa ukilenga kuikatisha, kwanza unajitengenezea madhara kwa kutengeneza usugu wa dawa hiyo mwilini mwako.”


Anasema, "Ukimeza dawa bila kuumwa, ile dawa inatengeneza usugu, siku utakapoumwa na unapaswa kuitumia dawa hiyo haiwezi kukutibu tena."


Dk Mkeyenge anasema hedhi huanzia ndani, hivyo hata kwa watakaotumia ndimu au limao ili waikate inaweza kutooneka kwa nje lakini baadaye itaendelea na si njia nzuri kufanya hivyo.


Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Morogoro, Daniel Nkungu anasema kitaalamu hakuna njia kama hizo na athari zake kwa wanaofanya hivyo zinaweza kusababisha madhara kwenye mfumo wa uzazi.


"Njia hizo zinaweza hata kuathiri mfumo wa uzazi na huyo anayefanya akashindwa kuzaa kama vitu anavyotumia kuweka ukeni vitapanda na kwenda kwenye mayai. Hii ni hatari, ni bora kama mtu ana shida na hedhi kwenda hospitali," anasema.


Dk Nkungu anasema kuna dawa za kuahirisha hedhi ambazo hutolewa kwa mtu maalumu, tena kwa kuthibitishwa na daktari.

Baadhi ya hao anasema ni wenye uvimbe mkubwa wanaopaswa kufanyiwa operesheni au wanaotoka damu mfululizo.


"Ninachofahamu kitaalamu kama mtu ana tatizo kuna dawa ambazo wakati mwingine hutumika kwenye uzazi wa mpango, ambazo zinaahirisha hedhi,” anasema na kuongeza:


“Hakuna njia kitaalamu inayoathiri hedhi, hata hizi dawa ninazosema huwa zinazuia damu isitengenezwe au isitoke kwa muda fulani, ikiisha hedhi inarudi na hapewi kila mtu.”


Daktari mwingine bingwa wa maradhi ya wanawake, jijini Dar es Salaam, Isaya Mhando anasema wanaotumia ndimu au limao wana tatizo la elimu ya afya ya uzazi.


"Kuweka vitu kama hivyo ukeni kunasababisha vitu vingi, ikiwamo kuharibu kinga inayozuia bakteria waharibifu na fangasi wasiingie kule,” anasema.


Dk Mhando anasema, "Unaharibu mazingira ya wale bakteria na kinga ya mazingira ya uke inapotea, ndiyo sababu kuna wengine wanatoka uchafu na wapo wengine hata kama hawatoki uchafu lakini uke unatoa harufu kali mithili ya shombo la samaki.”


Anasema hakuna sayansi ya kuzuia hedhi kwa ndimu au limao na kwamba, hata wanaodai kutumia flagly, swali la kujiuliza ni, “dawa hiyo hutibu nini na wewe unameza ili kutibu nini?”


Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad