Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Komredi Abdulrahman Kinana amezindua Ofisi za kisasa za Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambapo ujenzi wa Ofisi hizo umeenda sambamba na ujenzi wa mgahawa wa kisasa.
Uzinduzi huo umefanyika hii leo Desemba 13, 2023 katika Ofisi za CCM Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita, huku akimpongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa kubuni na kuleta mawazo hayo ya ujenzi ambayo yalienda Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu na baadaye Wanachama na hivyo uamuzi wa kujenga majengo hayo ulifanyika.
Amesema, “hamuwezi kuunda na kuimarisha muundo wa Chama kama hamna ofisi za kufanyia kazi na ukumbi wa kufanyia shughuli zenu badala yake kunapokuwa na mikutano mnakodisha kumbi nyingine na viongozi hawana ofisi, hivyo leo mmetekeleza Ibara muhimu ya Ilani inayotaka WanaCCM kukiimarisha, kujijenga Chama Kitaasisi kwa kuwa na Ofisi na zana za kufanyia kazi.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Dkt. Doto Biteko amemshukuru Komredi Kinana kwa heshima aliyowapa CCM Bukombe ya kuzindua Majengo ya Ofisi, Wadau waliochangia katika ujenzi wa majengo hayo wakiwemo WanaCCM wenyewe ndani ya Wilaya ya Bukombe, Wananchi wa makundi mbalimbali, baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali.