Kipa wa Tabora United Mnigeria, John Noble amesifu uwezo wa nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki aliouonyesha katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo kukutana msimu huu uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Katika mchezo huo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lililofungwa na Aziz Ki katika dakika ya 21 na kuifanya timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kupoteza mechi yake ya nne kati ya 13 ilizocheza ikishinda tatu na kutoka sare sita ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo na pointi 15.
Akizungumza na Mwanaspoti, kipa huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Enyimba ya NIgeria, amesema wakati mpira unapigwa na Aziz Ki kulikuwa na mwanga wa taa uliopiga kwenye macho yake hivyo kushindwa kuona vizuri na kuruhusu bao.
“Kwanza nasifu uwezo wake kwa sababu alitumia maarifa wakati anaupiga, ni kweli nilizidi mbele kidogo ya lango langu ila sio kigezo cha kuacha kumsifia mpigaji, tulijiandaa vizuri kushinda mchezo lakini bahati haikuwa upande wetu,” alisema.
Noble aliongeza pia kutoka kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora na kutumia Jamhuri kama wa nyumbani kwa kiasi kikubwa kuliwaathiri.