Dar es Salaam. Kama kwako Krismasi ilikwenda sawa ni jambo la kumshukuru Mungu, maana wapo iliyowaacha na huzuni, ikiwamo familia ya Isaya Ndindindi, iliyopoteza vijana wawili katika ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Vijana hao, Elisha Isaya (18) na Richard Robert (14) wamefariki dunia walipojaribu kuvuka mkondo wa bahari hiyo ili wakaogelee karibu na fukwe ya South eneo la Mjimwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, kabla ya vijana hao kwenda ufukweni, walionywa kwamba ni maeneo hatari kwa usalama wao.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limethibitisha vifo vya vijana hao.
Mbali ya wawili hao kupoteza maisha, limesema halijapokea taarifa nyingine mbaya iliyotokea wakati wa Sikukuu ya Krismasi.
Akisimulia tukio hilo la jana Desemba 25, 2023, dada wa marehemu, Pili Isaya anasema ndugu zake walitoka nyumbani kwenda ufukwe muda mchache baada ya chakula cha mchana.
“Hawakuwa nyumbani. Walikuwa eneo la jirani, chakula kilipokuwa tayari waliitwa kuja kula,” anasema Pili.
“Baada ya kula mama aliwaambia wasiende baharini, kwani wanaweza kupatwa na tatizo lolote, lakini walipigiana simu na wenzao wakaamua kwenda bila taarifa,” anasema.
Anasema tangu walipoonekana wakati huo, hawakuwaona tena hadi saa 11 jioni, vijana waliokuwa nao baharini waliporudi nyumbani kutoa taarifa kwamba wamezama.
Mashuhuda
Aboubakar Ismail, anasema safari yao kwenda baharini ilitokana na simu aliyopokea kutoka kwa rafiki yake Elisha (sasa marehemu).
“Elisha alinipigia simu akasema twende baharini tumpeleke mgeni (Richard ambaye pia ni marehemu) kuona mazingira na tukaogelee naye, tukaenda tukiwa wanne,” anasema.
Anasema kabla ya kufika eneo ambalo watu wengi hulitumia kuogelea, inakupasa kuvuka mkondo wa maji.
Anaeleza walipofika eneo hilo, Elisha aliwaambia anajua kuogelea, hivyo ataanza kumvusha mgeni kisha atawarudia wengine.
Harakati za kumvusha mgeni zilianza, amesema baada ya kufika katika kina kirefu Richard alikunywa maji na ndipo alipomkumbatia Elisha.
Wakiwa katika hali ya kukumbatiana, Ismail anasema wawili hao walishuhudiwa wakizama na kuibuka ndani ya kina hicho kirefu cha maji.
Ismail anasema alijitosa majini kujaribu kuwaokoa, lakini alishindwa kwa kuwa hawezi kuogelea.
Anasema mwenzao naye alijitosa majini, lakini pia hakufanikiwa kwani alipowafikia, Richard alishikilia nguo yake kiasi cha kushindwa kutoka.
“Richard alimshika nguo mwenzangu ikabidi aivue ili ajiokoe, akafanikiwa kutoka. Tulipoona tunashindwa tukaenda kutoa taarifa kwa wavuvi waliokuwa jirani. Wakati wanaendelea kuwatafuta, tulirudi nyumbani kutoa taarifa,” anasema.
Ismail anasema walipofika eneo la tukio wakiwa na familia hawakuona chochote, hivyo taarifa zilitolewa kwa Jeshi la Polisi.
Saa tano baadaye, anasema mwili wa Richard ulionekana kando mwa fukwe, huku mwili wa Elisha ulionekana saa 11 alfajiri ya kuamkia leo Desemba 26, 2023.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo amesema tahadhari ilitolewa kabla ya sikukuu kuhusu watu wanaokwenda kujifunza kuogelea.
“Haiwezekani hujui kuogelea eti siku ya sikukuu ndiyo uende kuingia kwenye maji kuogelea. Tulitoa tahadhari mapema kuepuka madhila kama haya,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu matukio mengine katika sikukuu hiyo, Murilo amesema hajapokea taarifa nyingine yoyote.
“Mkoa wa Dar es Salaam upo shwari sijapokea taarifa nyingine yoyote, kikubwa watu wazingatie tahadhari tunazotoa wakati huu wa sikukuu,” amesema.