Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Saimon Msuva. WANANCHI kuna bomu wanataka kulitengeneza kupitia dirisha hili dogo la usajili nalo ni kushusha mashine za kazi kwa ajili ya kuifanya timu hiyo kuwa tishio mara baada ya eneo la ushambuliaji kuonekana kupungukiwa na makali.
Yanga kwenye eneo la ushambuliaji la timu lipo chini ya washambuliaji watatu wa kati ambao ni Kennedy Musonda, Clement Mzize na Hafiz Konkoni ambao kwa sasa wamekuwa na uwiano mbaya wa kutupia mabao.
Tayari championi Ijumaa limenasa taarifa za Yanga kumrudia tena mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Saimon Msuva baada ya kupata taarifa za mshambuliaji huyo kuachana rasmi na klabu yake ya JS Kabylie ya nchini Algeria baada ya kuitumikia kwa mizei minne pekee.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga pia zimelielezea Championi Ijumaa kuwa, Msuva baada ya kutoka Saudi Arabia ilibaki kidogo ajiunge na Yanga kabla ya kwenda zake Algeria kucheza soka la kulipwa.
Mabosi wa Yanga kwa sasa wameanza harakati za kutaka kumsajili tena ili aweze kuisaidia timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa ambapo kikosi hicho kipo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Dirisha kubwa lililopita baada ya Msuva kutoka Saudi Arabia Yanga walionyesha nia ya kutaka kumsajili na walikuwa kwenye mazungumzo ya muda mrefu jambo ambalo hata hivyo lilishindikana, sasa baada ya taarifa za JS Kabylie kuachana na mshambuliaji huyo mabosi wamerudi tena kutaka kumsajili.
“Kikubwa kwa sasa ngoja tuone nini kitatokea lakini ukiachana na Msuva bado kuna wachezaji wengine ambao pia Yanga walikuwa kwenye hatua nzuri za kutaka kuwasajili hivyo muda ndio kila kitu tusubiri na tutafahamu,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally kamwe kuhusiana na usajili wa Msuva kuhitajika na Yanga alisema kuwa: “Kwa sasa niweke wazi kuwa Yanga itashusha mshambuliaji wa maana, siwezi kusema ni mshambuliaji gani lakini lazima niweze kusema kuwa watu wataushangaa sana usajili wetu.
“Ni usajili wa akili,watu wanapomuona Rais wetu Injinia Hersi anazunguka nchi mbalimbali wanaona kama anaenda kutalii tu, niwaambie kuwa huwa yupo kazini na tayari ameshafanya ziara nyingi sana na huko ameweza kujipatia wachezaji wa maana na muda si mrefu mtawaona na watawaburudisha maana ni wachezaji wa maana kweli kweli.”
Mbali na Msuva Yanga pia inahusishwa na nyota wengine kibao wa kimataifa ambao ni winga wa FC Lupopo ya DR Congo, Manu Labola Bota ambapo kama Yanga watamnasa pamoja na Msuva basi safu ya ushambuliaji ya Yanga itakuwa na wachezaji hatari.
Hiyo ni kutokana na uwepo wa wachezaji kama Pacome Zouzoua ambaye kwa sasa ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye michuano ya kimataifa ndani ya Yanga akiwa amefunga mabao 3 huku kinara akiwa ni Karamoko Sankara wa Asec ambaye ana mabao 4.
Faida ya Yanga endapo wataipata saini ya Msuva ni kwamba mchezaji huyo pia ana uwezo mkubwa wa kucheza kama winga wa kushoto na kulia lakini pia kucheza kama namba 9 na namba 10 jambo ambalo litakuwa faida kwa Kocha Miguel Gamondi kwenye kufanya uchaguzi wa wachezaji wa kucheza mechi.
Kwa upande wa Manu Labola Bota pia anauwezo wa kucheza winga zote za pembeni kwa maana ya kushoto na kulia pia akiwa na uwezo mkubwa wa kufunga kutokea pembeni kama ilivyokuwa kwa Pacome.