Kwa nini Simba Wasiachane na Clatous Chama?

Kwa nini Simba Wasiachane na Clatous Chama?


Hakuna kitu kibaya kama kutoaminika kwenye maisha. Simba na Clatous Chama wamekuwa na ndoa ya muda mrefu, lakini hakuna anayemuamini mwenzake. 


Ni kweli Chama bado ni mchezaji mzuri na anaweza kwenda kwenye kikosi cha kwanza cha timu yoyote hapa nchini. Huku kushuka kwa kiwango kunakoonekana siku za hivi karibuni ni kwa sababu Simba pia imeshuka. Chama bado ni mchezaji mzuri na kwa ligi yetu bado ana misimu miwili au mitatu mbele ya kusumbua.


Chama anawasumbua sana Simba kwa sababu ndiye staa mkubwa kwenye timu aliyetawala muda mrefu. Amekuwa na kiburi. Amekuwa na maringo kila kukicha. Lakini, Simba pia ni kama hawamuamini sana.


Kuna namna wanamuona kama msaliti. Kuna namna wanamuona kama mtu ambaye huwa hajitoi sana hasa kwenye mechi dhidi ya Yanga. Chama pia kila dirisha la usajili amekuwa akihusishwa kwenda Yanga. Kwa tamaduni za mpira wetu ndoa ya Chama na Simba haina mwisho mzuri.


Ukishakuwa na mchezaji tegemeo ambaye humuamini ni bora kuachana naye ili maisha yaendelee. Ukishakuwa na mchezaji ambaye kila msimu ni lazima asumbue bila hata sababu za msingi ni bora uachane naye. Nadhani kulinda heshima ya Chama na mchango wake pale Simba na kwa maslahi ya klabu, ni bora pande hizi mbili zikaachana.


Tuhuma za kila siku kucheza chini ya kiwango hasa mechi dhidi ya Yanga kuna muda zinamkosea pia adabu Chama. Hizi ni tuhuma nzito ambazo hazijawahi kuthibitishwa. Kama unamtuhumu mchezaji kila siku na huthibitishi madai yako, huko ni kumkosea adabu. Hali ikishakuwa hivi, ni bora pande mbili kuachana.


Chama amekuwa mfalme pale Simba kwa muda mrefu. Walau wakati yupo Luis Miqussone kwenye ubora wake, ilikuwa inasaidia. Chama kila siku ni tuhuma na shutuma tu na waajiri wake. Pale Manchester United walimrudisha Cristiano Ronaldo kwa furaha kubwa kama Chama alivyorudi Simba.


Baada ya hapo, Cristiano kila siku anasumbua timu. Mara leo kasusa hiki, mara kesho kaja na jambo lingine. Unajua kilichotokea? Klabu iliamua kukaa naye mezani na kumalizana.


Manchester United ni kubwa kuliko mchezaji yeyote. Sio kwamba Manchester United hawakuwa wanamhitaji Cristiano. Hapana. Waliamua kulinda heshima ya klabu. Kuondoka kwa Cristiano hata kama uwanjani ubora umepungua, lakini kibiashara kuna namna imewaumiza Manchester United. Chama bado ana uwezo wa kutoa mchango kwenye timu lakini haizuii kuachwa. Hakuna mchezaji mkubwa kuliko Simba.


Simba inahitaji kuwa na wachezaji wanaoiwaza zaidi timu kuliko wao binafsi. Simba ina wachezaji wengi wa kigeni lakini ni kwanini kila siku wanaona kama Chama anawasaliti? Haiji kwa bahati mbaya. Moja kati ya vitu vigumu ambavyo nadhani Simba wanahofia ni kumuona anakwenda Yanga.


 Hapa ndipo pagumu. Kila wakiwaza kwamba wakitangaza tu kuachana naye atakwenda kwa watani wanarudi nyuma. Binafsi sio tatizo kama Simba wataachana naye na akakiunga Yanga. Simba ilikuwepo. Ipo na itaendelea kuwepo. Wachezaji wanakuja na kuondoka.


Ujenzi wa Simba mpya na imara unahitaji uamuzi mgumu. Hata akienda Yanga, wamuache tu aende. Ukiachana na mwanamke usimchagulie bwana. Ni vyema kwa timu kama Simba ambayo inaanza kujitafuta upya baada ya kikosi chake cha dhahabu kupungua uwezo kuwa na watu wafia timu.


Ni kweli Chama bado ana kitu na akienda Yanga atakwenda kuwaongezea nguvu, lakini Simba itabaki kama Simba tu. Walishaondoka wachezaji wengi na timu ikabaki.


Hakuna haja ya kuendelea kuwa na mchezaji ambaye humuamini. Kuna muda utakuwa unamuonea bure. Kuna shutuma utakuwa unampa za bure. Ni vyema kila mtu akabaki salama. Chama naye ni kama kila mwisho wa msimu anatishia kuondoka. Kila msimu mpya lazima ahusishwe kwenda Yanga.


Haya nayo sio maisha. Ni sawa na kuwa na mke ambaye kila ikikaribia sikukuu anatishia kwenda kwa bwana mwingine. Maisha yakishafikia huko ni bora kuachana hata kama mnapendana. Huu ni muda wa mashabiki wa Simba kujifunga mkanda. Kukubali ukweli kuwa timu inahitaji utu na utulivu kusukwa upya. Zama zinapita kwa wachezaji wao wengi waliokuwa tegemeo.


Kıpindi kama hiki, sio cha kubembeleza wachezaji wasumbufu. Ni muda wa kuwaondoa na kuleta watu wapya. Hawa kina Pacôme Zouzoua hatukuwajua kabla, lakini wapo sokoni. Hawa kina Maxi Nzengeli hatukuwajua kabla, lakini wapo sokoni. Simba ni kubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote.


Mambo ya kubembelezana nadhani yamepitwa na wakati. Najua na wewe umekuwa ukifuatilia mwenendo wa Chama na Simba, nipe pia maoni yako. Nitumie tu ujumbe wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Njoo tuzungumze. Wachezaji wazuri wapo kila kona.


Ni Simba tu kujipanga vizuri. Yanga msimu uliopita wamepoteza karibu wachezaji watano tegemeo, lakini bado wako imara. Unajua kwanini? Wanajitahidi sana kwe-nye dirisha la usajili.


Sio kwamba wao hawakosei, hapana. Kuna usajili wanakosea isipokuwa, wanapatia mara nyingi na hasa misimu hii miwili. Kwa tafsiri yangu, Chama anajiwaza zaidi yeye kuliko klabu na klabu haijawahi kumuamini Chama hasa kwenye mechi dhidi ya Yanga tangu aje kwa mara ya kwanza.


Hakuna haja ya kuwa na ndoa ya mashaka. Ni bora kuachana kila mtu ashike hamsini zake.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad