Matumaini ya kuanza uzalishaji wa nishati ya umeme katika mradi wa bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) yanaendelea kuimarika, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuanza majaribio ya mitambo itakayozalisha nishati hiyo.
Mitambo imeanza kufanyiwa majaribio kwa kuingizwa maji na majaribio hayo yanatarajiwa kukamilika Februari 19, 2024 na baadaye utaanza uzalishaji wa umeme.
Mradi JNHPP unaogharimu zaidi ya Sh6.5 trilioni ukikamilika utazalisha megawati 2,115 na kuifanya Tanzania yenye mahitaji ya megawati 1,363.9 iwe na umeme wa kutosha.
Leo Alhamisi, Desemba 28, 2023, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametembelea mradi huo uliopo katika ya mikoa ya Pwani na Morogoro, akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga na baadhi ya watendaji wa Tanesco.
Amesema kwa hali ilivyo, kuna matumaini makubwa ya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika.
“Kwa mikakati tuliyoiona na wakandarasi wetu, usimamizi mzuri uliopo tutakamilisha shughuli hii kwa kipindi tulichopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ili kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.
“Mipango ya awali bwawa lilikuwa lianze kuzalisha umeme ifikapo Juni, 2024, lakini wakandarasi wameharakisha mchakato kutoka mwezi wa sita hadi Februari na tunaweza kukamilisha majaribio ya mitambo hii,” amesema Dk Biteko.
Kwa mujibu wa Dk Biteko, bwawa hilo limeshajaa maji mita 166.65 kutoka usawa wa bahari wakati kiwango kinachohitajika ni mita 163.
Dk Biteko amesema wingi huo wa maji umeharakisha hatua ya kuzalisha umeme tofauti na mipango ya awali ya kuanza shughuli hiyo Juni mwakani.
“Niwahakikishie Watanzania mradi huu lazima uwe jawabu la matatizo ya umeme tulioyanayo, Tanzania inakuwa kwa kasi maendeleo ya watu yanakuwa kwa kasi pia,” amesema Dk Biteko.
Dk Biteko amesema baada ya kukamilika kwa mradi huo, watahamia kuviendeleza vyanzo vya umeme vikiwemo vya jua na upepo, ili kumaliza tatizo la umeme kwa miaka 15 au 20 ijayo.
Aidha, amesema ujenzi wa mradi huo umefika asilimia 94.78, mashine mbili ambazo ni namba nane na saba za kuzalisha umeme megawati 470 zimeshafungwa. Amebainisha kuwa mashine nyingine zitafungwa kadri muda unavyokwenda.
Desemba 17, 2023 akizungumza na wafanyabiashara, wazalishaji na wamiliki wa viwanda, Rais Samia alisema Januari 2024 kinu cha kwanza kati ya tisa vilivyopo katika mradi wa JNHPP vitaanza uzalishaji vitawashwa kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa nishati hiyo.
“Pamoja na jitihada nyingine za gesi, sola (umeme wa jua) na mambo mengine, katika umeme wa hydro (maji), tunategemea nadhani katikati ya mwakani malalamiko yatakuwa yamepungua,” alisema Rais Samia.