Man City kumsaka mbadala wa Haaland

Man City kumsaka mbadala wa Haaland


Klabu ya Manchester City inafikiria kuingia sokoni dirisha la Januari 2024, kusajili Mshambuliaji mpya endapo Erling Haaland ataendelea kusumbuliwa na maumivu ya mguu.


Haaland alilazimika kuukosa mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Luton Town kwenye Ligi Kuu England mwishoni mwa juma lililopita na Kocha Pep Guardiola alisema mshambuliaji wake huyo anasumbuliwa na maumivu ya mguu.


Guardiola amesema Mshambuliaji huyo atahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na kutazama maendeleo yake siku kwa siku au wiki kwa wiki ili kujua ukubwa wa tatizo.


Haaland anatarajia kukosa mechi ya mwisho Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, ambapo Man City itakipiga na Red Star Belgrade huko Serbia, baadae leo Jumatano (Desemba 13), lakini Kocha Guardiola anaamini staa wake atakuwa tayari kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Dunia itakayofanyika huko Saudi Arabia, Desemba 19.


“Siku iliyofuata baada ya ile mechi ya Aston Villa, Haaland hakuwa anatembea vizuri” alisema Guardiola na kuongeza.


“Nilizungumza naye alisema anaendelea vizuri, lakini daktari alisema anahitaji kufanyiwa uchunguzi kwa ukaribu zaidi.”


Hata hivyo, Man City itaingia sokoni kusaka Mshambuliaji mpya kwenye dirisha la Januari 2024, kwa kile kinachoelezwa kama Haaland ataonekana kuwa na shida kubwa.


Haaland amekuwa muhimu kwenye kikosi cha Man City akifunga mabao 71 katika mechi 75 alizocheza za michuano yote.


Amekosa mechi nne tu za Ligi Kuu England tangu alipojiunga na Man City na tayari ameshafunga mabao 50, yakiwamo 14 aliyofunga kwenye mechi 15 alizocheza msimu huu 2023/24.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad