Nchini Afrika Kusini anajulikana kama Bulelwa Mkutukana, lakini dunia inamtambua kama Zahara. Mmoja wa wanamuziki wa kike wa Afrika Kusini waliofanikiwa kuiteka dunia na hisia za wapenda muziki.
Amejikusanyia mashabiki wengi duniani kutokana na kipaji chake na uwezo mkubwa wa kutuliza hisia za mashabiki.
Ni miongoni mwa wasanii wa kike waliofurahia matunda ya vipaji vyao na mwaka 2011 alikuwa miongoni mwa wanawake 100 waliotajwa kuwa na ushawishi duniani na BBC.
Hata hivyo, akiwa na miaka 36 tu, supastaa huyo wa muziki wa Pop Afrika Kusini, Zahara ameaga dunia wakati madaktari wakipambana kujaribu kuokoa maisha yake.
Zahara aliyetamba na kukusanya mashabiki wengi zaidi kupitia albamu yake ya Loliwe, amefariki dunia jana usiku kwenye hospitali moja jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Waziri wa Sanaa, Michezo na Utamaduni wa Afrika Kusini, Zizi Kodwa amesema kuwa Zahara alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya ini yaliyotokana na unywaji pombe kupita kiasi.
“Tuna majonzi ya kumpoteza Zahara, kwa kiasi Serikali ilikuwa naye bega kwa bega kusaidia familia yake kwenye matibabu. Tuko pamoja na familia yake. Tumempoteza Zahara na gita lake ambao walikuwa na mchango mkubwa kwenye sanaa ya Afrika Kusini,” amesema Kodwa.
Mapema mwezi uliopita, Meneja wa Zahara, Oyama Dyosiba alijitokeza hadharani na kukiri kwamba, supastaa huyo aliyevunja rekodi ya mauzo ya albamu ya Loliwe mwaka 2020 ikiwa ni miaka kadhaa baada ya kuiachia sokoni, ni mgonjwa na anapambania uhai hospitalini.
Mwaka 2019, dada mkubwa wa Zahara, Nomande alifichua kuwa familia ilipewa angalizo na madaktari kuhusu mwenendo wa unywaji pombe za msanii huyo kuwa unatishia uhai wake.
“Daktari ameniambia kuwa kama Zahara ataendelea kunywa pombe kupita kiasi anaweza kupoteza maisha. Kama familia tulikuwa na jukumu la kila kumdhibiti asitumie pombe. Tulipambana kuhakikisha hanywi pombe tena,” alisema wakati wa mahojiano.
Kwenye anga za muziki ndani ya Afrika Kusini na kimataifa, Zahara aliibuka na staili yake ya kipekee ya kuimba huku akipiga gitaa, jambo lililompa umaarufu mkubwa.
Umahiri wake wa kuimba kwa hisia na suati yenye kupanda na kushuka, iliwafanya baadhi ya mashabiki wa muziki kumuona kama mrithi sahihi wa Brenda Fassie kwa Afrika Kusini.
Albamu yake ya Loliwe ilishinda Tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka nchini Afrika Kusini huku mwaka 2013 alipata nafasi ya kutuimbuiza nyumbani kwa Nelson Mandela kabla ya baba wa Taifa hilo hajaaga dunia.
Zahara alizaliwa Novemba 9, mwaka 1987 na kama ilivyo kwa wasanii wengine duniani, kipaji chake kilianza kuonekana akiwa bado binti mdogo. Albamu yake ya kwanza ya Loliwe akiwa chini ya lebo ya TS Records ilitoka mwaka 2011. Hata hivyo, miaka kadhaa baadaye ilikuja kuwa maarufu zaidi na hapo akajulikana kila kona.
Pia, ana albamu ya Phendula iliyotoka mwaka 2012 yenye nyimbo za Impilo, Stay na Phendula yenyewe. Mwaka 2015 aliachia albamu yake ya tatu ya Country Girl na hapo akaachana na TS Records na kuwa chini ya Warner Music alikovuna fedha nyingi zaidi.
Akiwa na Warner alirekodi albamu za Mgodi mwaka 2017 na Ngaba Yam ya mwaka 2021 ikiwa albamu yake ya tano na ya mwisho. Enzi zake za uhai Zahara ameshinda tuzo 17 tofauti na amewahi kuwa Jaji wa Shindano la Idols Afrika Kusini.