Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anatarajiwa kuzuru mkoani Manyara kesho Desemba 7, 2023 kuwatembelea waathirika wa tukio la maporomoko ya tope lililotokea wilayani Hanang.
Katika ziara hiyo Mbowe atazitembelea familia zilizokumbwa na kadhia hiyo iliyotokea alfajiri ya Desemba 3, mwaka huu.
Katika tukio hilo, sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu ilinyonya maji ya mvua na kutengeneza tope ambalo liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 65 na kujeruhi wengine 117.
Maporomoko pia yameharibu miundombinu ya Barabara, maji na umeme pamoja na makazi ya watu.
Taarifa ya Chadema ya leo Desemba 6, 2023 imeeleza katika ziara hiyo, Mbowe ataongozana na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini wa chama hicho, Godbless Lema na viongozi wengine wa Mkoa wa Manyara na wilaya zake.
“Atawatembelea majeruhi waliopo hospitali ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Hanang kuwapa pole. Pia atawatembelea waathirika waliopo kwenye kambi na familia zilizoathiriwa katika tukio hilo na Kijiji cha Gendabi kujionea hali halisi ya madhara yaliyojitokeza,” imesema sehemu ya taarifa ya Chadema.
Uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini umewaomba Watanzania wote na hasa waliopo kwenye mikoa ndani ya kanda hiyo kujitokeza kutoa nguvu kazi kusaidia juhudi za uokozi.
Pia wameombwa kutoa misaada ya utu na faraja kwa ajili ya familia zilizoathiriwa na mafuriko.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, Rais Samia Suluhu Hassan pia atawatembelea waathirika hao kesho.
Tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri wamezuru mkoani Manyara.
Majaliwa alitoa maelekezo na miongozo kadhaa katika uokoaji na kurejesha miundombinu iliyoharibika katika hali ya kawaida.