Pacome Zouzoua ameendelea kuongeza akaunti ya mabao kwa kufikisha matatu nyuma ya Sankara Karamoko wa Asec Mimosas mwenye mabao manne, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeama ya Ghana kwenye Uwanja wa Mkapa huku Pacome akihusika na bao moja kati ya matatu na hivyo kuingia kwenye vita ya mabao na Sankara.
Pacome alifunga bao hilo dakika ya 33 baada ya kupokea pasi ya Khalid Aucho kisha kukokota mpira na kuwahadaa mabeki wa Medeama kabla ya kupiga shuti kali lililowapa faraja mashabiki na kuitoa timu kwenye presha kwani ni bao lililodumu hadi mapumziko.
Bao hilo lilimfanya apande hadi nafasi ya pili ya wafungaji wa hatua hiyo ya makundi nyuma ya Sankara mwenye mabao manne, kwani Pacome alifunga bao moja katika kila mechi (mbili) mfululizo zilizopita dhidi ya Al Ahly ya Misri na ule wa kwanza wa Medeama ulioisha kwa sare wiki iliyopita.
Pacome aliyesajiliwa na Yanga msimu huu, amekuwa moto na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo wamuimbe kutokana na ubora wake uwanjani.
Pacome pia ametupia kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara na hadi sasa amefunga manne na kutokana na ubora wake anatajwa kuwa mmoja wa wafungaji bora kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.