Mchezo wa Soka Ulivyoiheshimisha Tanzania Mwaka Huu 2023

 

Mchezo wa Soka Ulivyoiheshimisha Tanzania Mwaka Huu 2023

Matukio mengi yametokea katika mwaka 2023 katika sekta tofauti ambapo yapo ya kufurahisha na pia kuna yale ya kusikitisha.


Kwa mchezo wa soka, mwaka 2023 ulipitia nyakati tamu ambazo hapana shaka zinaacha kumbukumbu nzuri kwa mashabiki, wapenzi na wadau wa mchezo huo unaoongoza kwa kupendwa duniani.


Kufanya vizuri kwa timu mbalimbali za Tanzania za klabu na taifa kulifanya nyuso za wanafamilia wa mpira wa miguu ziwe na furaha na tabasamu kwa muda mrefu badala ya huzuni.


Spoti Mikiki inakuletea orodha ya matukio ambayo yalifanya soka liipe chati Tanzania kwa mwaka huu ambao unaelekea kufikia ukingoni.


Yanga Fainali Shirikisho Afrika


Baada ya kutolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iliangukia katika hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilipangwa kukutana na Club Africain ya Tunisia.


Iliitupa nje Club Africain kwa ushindi wa bao 1-0 na ikapangiwa kundi D la mashindano hayo na timu za Monastir, TP Mazembe na Real Bamako ambapo ilimaliza ikiwa kinara baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare moja huku ikipoteza moja.


Katika hatua ya robo fainali ikaitupa nje Rivers United kwa ushindi wa mabao 2-0 na kwenye nusu fainali ikapata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Marumo Gallants.


Kwenye fainali mambo hayakuiendea vizuri Yanga kwani ilikosa ubingwa mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni ya faida ya mabao ya ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.


Simba robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika


Kampeni ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa ilianzia kwa kufanya vizuri katika raundi mbili za mwanzo za mtoano ikizitoa Nyasa Big Bullets na Primiero de Agosto na kisha ikatua hatua ya makundi.


Ilipangwa kundi C pamoja na timu za Raja Casablanca, Horoya na Vipers ambapo ilimaliza katika nafasi ya pili ikishinda mechi tatu na kupoteza michezo mitatu.


Shughuli yake iliishia katika robo fainali ambayo iliyolewa na Wydad kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.


JKT Queens Klabu Bingwa Afrika


Maafande wa JKT Queens baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya wanawake Tanzania, walipata fursa ya kushiriki mashindano ya Baraza la Vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ya kuwania kufuzu fainali za klabu bingwa Afrika kwa wanawake.


JKT Queens iliitoa Tanzania kimasomaso katika mashindano hayo baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya CBE ya Ethiopia na hivyo kukata tiketi ya kuiwakilisha CECAFA katika mashindano ya Afrika.


Katika fainali za klabu bingwa Afrika, JKT Queens iliishia hatua ya makundi baada ya kupoteza mechi mbili na kupata ushindi katika mchezo mmoja.


Taifa Stars Afcon


Harakati za timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani huko Ivory Coast zilimalizika vyema mwaka 2023 baada ya kukata tiketi ya kucheza mashindano hayo.


Sare ya bila kufungana ugenini dhidi ya Algeria iliifanya Taifa Stars imalize hatua ya makundi ya kuwania kufuzu fainali hizo ikiwa katika nafasi ya pili kwenye kundi F baada ya kukusanya pointi nane nyuma ya Algeria iliyoongoza kundi hilo ikiwa na pointi 16.


Hiyo ni mara ya tatu kwa Taifa Stars kufuzu fainali hizo ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 1980 na mara ya pili ikiwa ni 2019 ambazo awamu hizo zote iliishia katika hatua ya makundi.


Idadi ya timu za taifa 24 ndizo zimefuzu kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Januari mwakani ambazo ni Ivory Coast, Morocco, Algeria, Afrika Kusini, Senegal, Nigeria, Burkina Faso, Tunisia, Misri, Zambia, Guinea ya Ikweta, Guinea Bissau, Cape Verde, Mali, Guinea, Ghana, Angola, Tanzania, Msumbiji, DR Congo, Mauritania, Gambia, Cameroo na Namibia.


Twiga Stars Wafcon


Ndoto iliyodumu kwa miaka 13 ya timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ilitimia rasmi Desemba 5 mwaka huu baada ya timu hiyo kufanya hivyo.


Twiga Stars ilifuzu fainali hizo baada ya kuitupa nje Togo kwa ushindi wa mabao 3-2, ikishinda mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza hapa Tanzania uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.


Katika mchezo wa pili, Twiga Stars ilipoteza kwa mabao 2-0 huko Rome, matokeo ambayo hayakutosha kuifanya Togo ifuzu mbele ya timu hiyo ya wanawake ya taifa ya Tanzania.


Kabla ya kufuzu awamu hii, mara ya mwisho ambayo ilikuwa pekee kwa Twiga Stars kushiriki fainali za Wafcon ilikuwa ni 2010 pindi zilipofanyika Afrika Kusini ambapo ilimaliza mkiani mwa kundi A ikiwa haina pointi, ikifunga mabao matatu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja.


Timu 12 ambazo zimefuzu fainali hizo za mwakani ambazo zitafanyika Morocco ni wenyeji, Afrika Kusini, Nigeria, Algeria, Ghana, DR Congo, Tunisia, Senegal, Botswana, Tanzania, Mali na Zambia.


Simba, Yanga makundi Ligi ya Mabingwa


Haikuwahi kutokea Tanzania kuwakilishwa na timu mbili kwa pamoja kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini mambo yamekuwa kinyume mwa 2023 ambapo hilo lilitokea na kumaliza historia ya unyonge wa nchi yetu kwenye mashindano hayo.


Hiyo ni baada ya Yanga na Simba kutinga kwa pamoja baada ya timu hizo mbili kufanya vyema kwenye hatua za mwanzo za mtoano za mashindano hayo.


Simba ambayo ilianzia raundi ya kwanza, ilifuzu baada ya kuitupa nje Power Dynamos ya Zambia kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 ambapo katika mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na marudiano hapa Dar es Salaam.


Yanga iliyoanzia raundi ya awali, iliitupa nje ASAS ya Djibouti kwa mabao 7-1 ambapo mechi ya kwanza ilishinda 2-0 na mechi ya marudiano ikashinda 5-1 na raundi ya kwanza ikaumana na Al Merrikh ya Sudan na kuitupa nje kwa ushindi wa mabao 3-0, ikishinda 2-0 katika mechi ya kwanza na marudiano ikapata ushindi wa bao 1-0.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad