Mechi ya Ushindi na Heshima Leo Yanga Vs Madeama

 

Mechi ya Ushindi na Heshima Leo Yanga Vs Madeama

“Leo ndio leo leo…” Huo ndiyo wimbo unaogonga kwenye mioyo ya mashabiki wa Yanga na kuanzia saa 10:00 jioni, chama lao litakuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mechi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Medeama, na mchezo wa kwanza ugenini iliilazimisha miamba hiyo ya Ghana sare ya bao 1-1, Desemba 8, mwaka huu.

Mchezo huo ni wa kufa ama kupona kwa Yanga kwani inahitaji ushindi ili kurejesha matumaini ya kumaliza nafasi mbili za juu kundi D ili kujihakikishia kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Kwa sasa kundi hilo lipo wazi kwa kila timu baada ya mechi tatu likiongozwa na Al Ahly ya Misri yenye alama tano ikifuatiwa na CR Belouizdad yenye pointi nne sawa na Medeama ya tatu huku Yanga ikiwa mkiani na alama mbili ilizovuna baada ya sare na Ahly nyumbani na Medeama ugenini.

Kwa maana hiyo hesabu za kwanza kwa Yanga leo ni ushindi ili ifikishe alama tano kabla ya kumalizana na Al Ahly ugenini na Belouizdad nyumbani mechi zitakazopigwa Februari, mwakani ambazo pia watatakiwa kuibuka na ushindi na kumaliza na pointi 11 zitakazowapeleka robo fainali.

“Tumefanya kila kitu kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo huu mazoezini na wachezaji. Tumeshamaliza maandalizi tunafahamu jukumu ni moja tu kuhakikisha tunapata ushindi kwa kuwa huu ni mchezo muhimu kwetu,” alisema Miguel Gamondi, jana.

NINI KIFANYIKE

Kwa namna mechi ya kwanza ya Yanga na Medeama ilivyokuwa, kitu cha kwanza inachopaswa kufanya Yanga ni kucheza kwa nidhamu na kujitahidi kutumia vyema nafasi zitakazopatikana.

Medeama ni timu inayocheza soka la kasi na nguvu jambo ambalo Yanga inapaswa kujipanga zaidi kukabiliana nalo, lakini ikiwa inatumia sana dakika 15 za kwanza kushambulia na 15 mwishoni mwa kila kipindi.

Akizungumzia mchezo huo, mchezaji wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema Yanga inatakiwa kuiheshimu Medeama na kucheza kwa tahadhari kubwa huku ikitafuta bao la mapema bila kuwaza inacheza uwanja wa nyumbani.

“Medeama sio timu ya kubeza. Tuliona walivyocheza mechi ya kwanza wana kasi, nguvu na morali ya juu jambo ambalo Yanga wanatakiwa kuliheshimu na kuwa tayari kukabiliana nalo. Lakini wakati wakifanya hivyo wanahitajika kuhakikisha wanapata bao mapema ili kupunguza presha,” alisema SMG.

Eneo ambalo Medeama imekuwa hatari zaidi ni katika mistari ya pembeni na imekuwa hodari kupita huko kutokana na ubora na mabeki wake wa pembeni Kwadwo Amoako na Mamadu Kamaradin ambao muda mwingi hupanda na kuongeza nguvu kwa mawinga Daniel Lomotey na Derrick Fordjour ambao wana kasi sana, hii ikiwa sehemu ambayo mabeki wa Yanga wanatakiwa kuwa makini nayo kwa kuwa ndiyo imekuwa inatengeneza nafasi za mabao.

Yanga inatakiwa kuwa imara zaidi maeneo hayo kuwadhibiti wachezaji wa Medeama kutofanya mikimbio sahihi.

Sehemu nyingine ambayo Medeama imetega silaha yake ya maana ni eneo la ushambuliaji wa kati na anacheza straika aliyefunga bao la timu hiyo kwenye mechi ya kwanza, Jonathan Sowah, raia wa Ghana.

Mwamba huyo amekuwa na nguvu, kasi na ubora wa kucheka na nyavu na hata kwenye mechi ya kwanza aliwasumbua kina Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job hivyo anatakiwa kuchungwa sana.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema Yanga isiingie uwanjani ikiwabeza Medeama kwani nao wanahitaji ushindi na wana timu bora. “Yanga iingie ikijua Medeama wanaitaka mechi hii, Waende wakijua watakutana na watu wagumu hivyo wacheze kwa nguvu zote huku wakitumia vyema faida ya mashabiki na uwanja wa nyumbani. Naamini itakuwa mechi nzuri na yenye ushindani na naona Yanga ina nafasi kubwa ya kupata ushindi,” alisema.

TAJIRI AFANYA KUFURU

Achana na kununua tiketi zote za viti vya mzunguko na kuzigawa bure kwa mashabiki watakaokuwa wamevalia jezi za Yanga, Mwanaspoti limepenyezewa mdhamini wa timu hiyo, Gharib Said Mohamed amewaahidi mkwanja mrefu wachezaji wa Yanga kama watashinda mechi hiyo.

Licha ya uongozi wa Yanga kushindwa kuweka wazi ni kiasi gani watavuna kutoka kwa GSM kama watashinda, lakini hadi tunaingia mitamboni ilikuwa ikifahamika si chini ya Sh300 milioni.

Huo umekuwa utaratibu wa GSM tangu aanze kuipa sapoti timu hiyo na mara ya mwisho kutoa mkwanja mrefu ni pale chama lake lilipoichapa Simba mabao 5-1 kumbuka ni tofauti na ile ambayo inatolewa na Yanga.

MWENENDO UKOJE?

Mwenendo wa timu zote mbili katika mechi zilizopita unaongeza ugumu mechi hiyo kwani zote zimefanya vyema kila moja katika nafasi yake. Medeama katika michezo mitano ya mwisho ya mashindano yote imeshinda moja dhidi ya Belouizdad na sare moja na Yanga huku ikichapwa mabao 3-0 na Al Ahly, 1-0 na Asante Kotoko na 1-0 na Berekum Chelsea. Yanga katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na 1-0 mbele ya Coastal Union ikitoka sare mbili dhidi ya Ahly na Medeama na kupoteza 3-0 kwa Belouizdad.

Kwa maana hiyo Yanga ina nafasi kubwa mbele ya Medeama hususan ikiwa Uwanja wa Mkapa kwani mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa 2016 katika mechi ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na baadaye ugenini Yanga ikachapwa 3-1.

Yanga itakuwa na faida ya kurejea kwa beki wa kushoto, Joyce Lomalisa aliyeikosa mechi ya mkondo wa kwanza kutokana na majeraha madogo aliyoyapata lakini pia mastaa wake wote tegemeo ambao baadhi yao walipumzishwa kwenye mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar akiwemo Stephene Aziz Ki, Pacome Zouzou, Djigui Diarra watakuwepo kuhakikisha jeshi la kocha mwenye misimamo, Miguel Gamondi linapata ushindi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad