MBWANA Ally Samatta anaelekea ukingoni mwa maisha yake ya soka baada ya miaka mingi ya kufanya vizuri. Kuna tunachomdai Samatta? Hakuna.
Samatta ameweka historia nyingi ambazo itachukua miaka mingi kuvunjwa. Alikuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa nyota wa ndani. Alifanya hivyo akiwa na TP Mazembe. Akawa Mtanzania wa kwanza kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Thomas Ulimwengu mwaka 2015. Akawa mfungaji bora mwenza katika mashindano hayo pia. Ni rekodi nzuri.
Akawa Mtanzania wa kwanza kucheza soka nchini Ubelgiji akacheza kwa mafanikio kwenye klabu ya KRC Genk. Akaweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo. Akatwaa ubingwa wa Ubelgiji pia. Inafurahisha sana. Baada ya hapo akaweka rekodi ambayo itachukua muda mrefu zaidi. Akawa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England. Nani alifikiria hilo? Licha ya kwamba alicheza Aston Villa kwa muda mfupi, ila ndiyo ameacha alama kubwa.
Baada ya hapo kila mtu anafahamu kilichoendelea. Akaenda Uturuki kisha Ubelgiji tena. Sasa anacheza huko Ugiriki. Kwa kifupi ametembea nchi nyingi za Ulaya kuliko Mtanzania yeyote. Amecheza timu kubwa pia. Ni rekodi nzuri kwake na kwa nchi.
Huyu ndiye Mbwana Samatta. Akiwa kwenye ubora aliimbwa kama shujaa kwenye viunga vyote vya DR Congo. Alikuwa mfalme kule Lubumbashi na Kinshasa. Waliimba jina lake kila kona. Akiwa huko Ubelgiji aliimbwa kama shujaa. Mashabiki wa Genk walimuona Samatta kama mkombozi wao. Aliwapa furaha karibu kila wiki. Alifunga mabao muhimu kwa timu yao.
Huyu ndiye Samatta. Mchezaji bora wa nyakati zote kuwahi kutokea Tanzania.
Nyuma ya Samatta kukawa na Thomas Ulimwengu. Bahati mbaya kwake alipoondoka tu Mazembe na nyota yake ikafifia. Hakuweza kuwa mchezaji mkubwa tena. Kwa sasa amerejea nchini na amekosa ushawishi hadi kwenye kikosi cha Singida Fountain Gate.
Kisha Saimon Msuva akawa ndiye shujaa mwingine. Akaenda nchini Morocco kwenye klabu ya Difaa El Jadida. Akawa mchezaji muhimu wa timu hiyo. Akaweka ufalme wake huko Morocco.
Baada ya mafanikio akasajiliwa na wababe wa nchini humo, Wydad Casablanca. Njia ya Msuva ikawa nyeupe. Msuva akawa shujaa mwingine wa nchi nyuma ya Samatta. Kila mtu akaona safari ya Msuva kwenda Ulaya imekaribia. Bahati mbaya mgogoro wake na Wydad ukamrudisha nyuma. Akaenda Saudi Arabia, akarudi Algeria na sasa huenda akarejea nchini. Nyakati zinakwenda kasi sana.
Ukweli ni kwamba tuna wachezaji mahiri wanaoondoka. Hawa kina Samatta na Msuva hawana muda mrefu tena. Wanakaribia kufikia ukomo wa ubora wao. Ni ukweli mchungu kwao. Ni ukweli mchungu kwa nchi. Inasikitisha sana.
Ubaya ni kwamba wakati kina Samatta wanakaribia kuondoka bado hakuna mwanga mkubwa mbele. Kwa sasa anaonekana Novatus Dismas kama mfalme ajaye wa Taifa Stars? Nani mwingine.
Tulimtarajia_ Kelvin John angalau awe ameanza kuiva mpaka sasa. Nini kimetokea? Ni ngumu kuelezea. Kelvin ameshindwa kuwa mchezaji mkubwa licha ya kwenda Ulaya mapema.
Ni miaka mitatu sasa na ushee tangu amekwenda Ubelgiji ameshindwa kuwa na nafasi kwenye kikosi cha wakubwa cha KRC Genk. Amekosa nafasi kwenye kikosi cha Taifa Stars. Ukweli ni kwamba ukuaji wake umekosa matumaini. Huyu ndiye alitajwa kama mrithi wa Samatta.
Kwa ligi ya ndani ndiyo kumekuwa na shida kubwa zaidi. Wakati John Bocco na wengineo wakielekea kumaliza soka lao, hakuna mbadala wenye matumaini. Angalau kwa Bocco inaonekana kama Clement Mzize anakuja kuchukua mikoba yake, ila bado ana safari ndefu.
Vii kuhusu wengine? Hakuna. Wachezaji wengi wazawa wamekuwa kwenye viwango vya kawaida. Ligi yetu sasa inabebwa zaidi na wachezaji wa kigeni.
Hawa kina Jonas Mkude, Sure Boy wanaondoka lakini hakuna viungo wa ndani ambao unaona wanaweza kuziba nafasi zao. Angalau katika mabeki tumekuwa na kizazi cha dhahabu cha kina Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca. Lakini maeneo mengi yamekosa wafalme wapya. Hii ndio sababu Shirikisho ka Soka Tanzania (TFF) linajaribu kutafuta watanzania wengine wanaocheza huko ughaibuni. Ndio tumewapata hawa kina Haji Mnonga, Ben Starkie, Charles Saimon na wengineo.
Nimeona kwenye mechi ya kirafiki pale Zanzibar kulikuwa na Watanzania wengine wapya katika timu yetu. Angalau wanaleta tumaini jipya. Ila ukweli ni kwamba itachukua muda kuziba nafasi zitakazoachwa wazi na kina Mbwana Samatta na Saimon Msuva. Wamefanya vizuri kwenye klabu zao na Taifa Stars. Wamekuwa wachezaji wa tofauti.
Kuna nyakati waliibeba nchini kwenye migongo yao. Nani ataifanya kazi hii baada yao? Ni jambo la kusubiri na kuona. Ila ukweli ni kwamba tuna changamoto kubwa katika hilo.
Unaweza kuwapenda watu
'Hakuna ubaya kwa mwanaume aliyeoa kucheza nje' - Mchungaji Elizabeth Mokoro