HATIMAYE Jeshi la Polisi limemkamata Lucas Paul Tarimo anayetuhumiwa kumuua kwa kumchoma visu 25 Beatrice James Minja, akiwa amejificha katika kijiji cha Jema kata ya Oldonyo Sambu Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha akijiandaa kukimbilia nchi Jirani. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Mtuhumiwa huyo amekamatwa leo Jumapili alfajiri ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Jeshi hilo litoe wito kwa wananchi kutoa ushirikiano ili Tarimo akamatwe.
Beatrice enzi za uhai wake
Taarifa iliyolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime imesema; “jitihada zilizoanza toka tarehe 12 Novemba 2023 liliporipotiwa tukio la Beatrice James Minja kuchomwa visu na hatimaye kufariki tarehe 27 Disemba 2023 katika Hospital ya KCMC zimezaa matunda.”
“Tunawashukuru sana wananchi wa kata hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa Jeshi la Polisi hadi kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ingawa baada ya kuona mkono wa serikali unamfikia alikunywa sumu inayotumika kuua wadudu, mtuhumiwa amepatiwa huduma ya kwanza yupo vizuri na taratibu za kisheria zinaendelea,” amesema.
Juzi Ijumaa Jeshi la Polisi lilijitokeza na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa taarifa kwa jeshi hilo ili kubaini alipo kisha kumkamata mtuhumiwa Lucas Tarimo.
Tarimo anadaiwa kumchoma visu na kumsababishia umauti Beatrice James Minja mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro ambaye alikuwa na mahusiano naye ya kimapenzi kabla ya wawili hao kuachana.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alikuwa anadaiwa kuwa msaidizi wa mashamba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda na mbunge wa Rombo lakini kiongozi huyo alikana kumfahamu ‘shamba boy’ huyo.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada mwanaharakati wa masuala mitandaoni, Godlisten Malisa kuchapisha kwenye akaunti yake ya Instagram taarifa ya mwanamke huyo aliyedaiwa kushambuliwa kwa visu 25 na Paul Tarimo aliyedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Beatrice.