Dar es Salaam. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu hatimaye wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliojiandikisha kupata vitambulisho vya taifa wanatarajia kuanza kuvipata kuanzia kesho Disemba 12.
Matumaini hayo yamekuja kufuatia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kutoa taarifa kwa umma inayowataarifu wakazi wa Jiji la Dar kujiandaa kupokea vitambulisho vyao.
Taarifa hiyo ya Nida iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano jana Jumatatu Desemba 11, 2023 imeeleza kuwa ugawaji wa vitambulisho kwa wilaya zote za Jiji hilo utaanza kesho na itadumu kwa siku 14.
“Wananchi wote waliosajiliwa na kupatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa (NINs) mnaombwa kujitokeza na kuchukua vitambulisho katika ofisi za Serikali za mitaa, ndani ya siku 14.
“Mwananchi atakayeshindwa kuchukua Kitambulisho chake ndani ya muda uliopangwa katika eneo lake, atalazimika kukifuata ofisi ya Nida ya wilaya anayoishi,” imeeleza taarifa hiyo.
Hili linakuja ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu Serikali ihaidi kulifanyia kazi suala la vitambulisho hivyo kwa kuhakikisha kila aliyeandikishwa anapata.
Septemba mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni akiwa katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Mtwara alisema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala la vitambulisho vya Nida na kufikia Machi mwakani kila aliyeandikishwa atakuwa amepata utambulisho huo.
Waziri huyo alisema Serikali imeshalipa fedha kwa mkandarasi anayetengeneza vitambulisho hivyo vya uraia.
“Katika bajeti iliyopita Serikali ilitenga Sh42.5 bilioni kwa ajili ya kutengeneza kadi milioni 11, fedha hizi zimeshalipwa kwa mkandarasi na anaendelea kuzitengeneza, baadhi tumeanza kuzipokea tunatarajia zote ziwe zimekamilia.
“Haitazidi Machi kadi zote zitakuwa zimepokelewa mwezi huu tumepokea kadi milioni 2 na tunaendelea kuzipokea kwa awamu kila mwezi hadi kufikia Machi mwakani hakutakuwa tena na ukosefu wa kadi,”alisema Masuni.