Paula Makonda Alia na Tanesco Kero ya umeme

 

Makonda alia na Tanesco kero ya umeme

Siku moja baada ya Wizara ya Nishati kusema kuwa kero ya kukatika kwa umeme inatarajiwa kuisha Januari 2024, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda amewataka watendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), kujitathmini utendaji wao kutokana na tatizo hilo.


Jana Desemba 20, 2023 Katibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba alisema tatizo la mgao wa umeme litakwisha ifikapo Januari mwaka 2024 baada ya mtambo mmoja wa kuzalisha umeme kutoka bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) kuanza majaribio ya kuzalisha umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.


Mramba amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua kiwango cha maji katika chanzo cha kuzalisha umeme cha Bwawa la Mtera lililopo wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.


Kauli kama hiyo pia imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, alipowakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda kuhusu upatikanaji wa umeme, akisema Januari mwakani kinu cha kwanza kati ya tisa vilivyopo katika mradi wa Bwawa la Nyerere kitawashwa na kuruhusu uzalishaji nishati hiyo.


Lakini akijibu maswali ya waandishi wa habari leo Desemba 21, waliotaka kujua, CCM inachukua hatua gani kwa tatizo la kukatika kwa umeme, Makonda ameitaka Tamesco kujiuliza maumivu anayopata Rais Samia, kuhusu changamoto ya umeme kama na wao wanayapata.


Amesema CCM inapeleka salamu kwa Tanesco kuhusu maumivu, mzigo uchungu na shauku anayoibeba Rais Samia katika kuhakikisha tatizo la umeme linakuwa katika historia.


“Wanamuacha Mwenyekiti wetu wa CCM (Rais Samia Suluhu Hassan), anayebeba peke yake, ukiona Rais anafanya mabadiliko au kuvunja bodi maana yake haivumuliki.


“Swali letu chama kwa watendaji wa Tanesco, kweli wanavyokaa huko walipo kelele, maumivu na sauti za Watanzania kuhusu umeme mnajisikia fahari? Kama mnajisikia fahari mnajiona mnastahili kumwakilisha Rais Samia, kama mnafaa kutoa huduma?” amehoji.


Makonda amesema zipo sababu zinazojulikana kuhusu changamoto ya umeme, lakini zingine ni uzembe tu, akisema kitendo cha mtendaji kukaa ofisi na kutoa maelezo bila kwenda eneo la tukio kinaleta taswira na mtazamo tofauti kwa Watanzania.


“Pamoja na jitihada zinazochukuliwa na mwenyekiti wetu (Rais Samia) na uamuzi mgumu wa kuvunja hadi bodi ya wakurugenzi wa Tanesco, chama kingetaka kuliuliza shirika hili, je wanadhani wanafaa kumwakilisha Rais?


“Kama leo hii Watanzania wakipiga kura sekta au kitengo chenu mngepata asilimia ngapi ili kutuongezea ushindi CCM, Januari kinu cha kwanza kinaanza kufanya kazi katika Bwawa la Julius Nyerere hii ni ahadi yao kwa Rais sasa iwe thabiti hakuna kulala, kulipana posho, tunataka umeme,”amesema Makonda. Desemba 19, 2023 Rais Samia alimteua Dk Rhimo Nyansaho kuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, akichukua nafasi Meja Jenerali Paul Simuli aliyeteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Uganda. Katibu huyo wa uenezi, amesema CCM haifurahishwi na mwenendo wa upatikanaji wa umeme, kwa sababu wanaona adha wanayoipata wananchi wa makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali wakiwemo mamalishe. Kwa nyakati tofauti kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa umeme ikiwamo kuwepo kwa mgao wa nishati hiyo usiofuata ratiba halisi inayoanishwa na shirika hilo. Makonda amesema ifike wakati kwa baadhi ya watendaji kama kazi wanaziona ngumu basi waache na kufanya jukumu jingine, pia aliwataka kujitathimini wenyewe kuliko kila mara kunapigiwa kelele.


Katika hatua nyingine, Makonda ametuma salamu kwa wanafamilia ambao ndugu zao ni watendaji wa Serikali, akiwataka wawaulize kama wanafaa kuwepo katika nafasi hizo za kumsaidia Rais Samia.


“Hizi ni salamu za CCM kwa ndugu zetu waliopo katika utumishi wao umma, tunataka kila mtu atimize wajibu wake, watu wote mnanifahamu ndio maana chama kimenileta hakuna kumbeba mzembe, mla rushwa na atakayeturudisha nyuma,” amesema Makonda.


Makonda ametumia nafasi hiyo kuwaonya baadhi ya makada walioanza harakati za kuusaka ubunge na udiwani, akisema wakati wao bado kwa sababu CCM ina viongozi wa nafasi hizo hadi mwaka 2025.


“Chama kina wabunge na madiwani, maelekezo ya CCM chokochoko zote zinazofanywa ziachwe, tuwape nafasi wabunge na madiwani walipo watekeleze majukumu yao, wakati ukifika tutatoa utaratibu.


“Kama kuna mtu aligombea au ana ndoto ya ubunge au udiwani, CCM inawatambua wabunge waliopo tuwape nafasi ya kutimiza majukumu yao, habari kupita pita sijui harambee au michango, sio sawa tunawanyima wabunge utulivu wao,” amesema Makonda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad