Polisi yafunguka sakata la Beatrice kuuawa kwa kuchomwa visu

 

Polisi yafunguka sakata la Beatrice kuuawa kwa kuchomwa visu

Jeshi la Polisi limejitokeza na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa taarifa kwa jeshi hilo ili kubaini alipo kisha kumkamata mtuhumiwa Lucas Tarimo anayedaiwa kumchoma visu na kumsababishia umauti mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Beatrice James Minja mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro.


Pia limeonya wananchi kujiepushe na taarifa za uzushi na uongo zenye malengo ya kuchafua watu wengine kwa nia binafsi.


Hatua hiyo imekuja saa chache baada mwanaharakati wa masuala mitandaoni, Godlisten Malisa kuchapisha kwenye akaunti yake ya Instagram taarifa ya mwanamke huyo aliyedaiwa kushambuliwa kwa visu 25 na Paul Tarimo aliyedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Beatrice.


Aidha, taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP – David Misime imesema mwanamke huyo aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC kwa bahati mbaya alifariki dunia tarehe 27 Disemba 2023 wakati akiendelea na matibabu.


“Jeshi la Polisi limeona taarifa hiyo ambayo kwa mujibu wa kumbukumbu ilitokea na kuripotiwa Polisi tarehe 12 Novemba 2023 na siyo tarehe 13 Novemba 2023.


“Taratibu za ufuatiliaji zilianza kwa kupata maelezo ya wanawake wanaodaiwa kuwa na Beatrice James Minja siku ya tukio ikiwa ni sambamba na kumtafuta mtuhumiwa ambaye alikimbia baada ya kutenda uhalifu huo.,” amesema Misime.


Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye jina lake sahihi ni Lucas Tarimo ambaye shughuli zake ni fundi ujenzi wa nyumba anazofanya katika maeneo mbalimbali ili akamatwe na taratibu zingine za kisheria zifuate kwani hakuna aliye juu ya sheria hata kama ana nafasi gani katika jamii au Taifa.


Aidha, ametoa rai kwa yeyote atakayemuona mtuhumiwa huyu asisite kutoa taarifa ili akamatwe.


Pia ametoa tahadhari kwa yeyote ambaye anamficha au anamsaidia kuendelea kujificha akibainika hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria.


“Tukio hili limemtokea binadamu na Mtanzania mwenzetu ni la kusikitisha na la kulaaniwa, tunasihi mwenye taarifa sahihi hata kama kuna uzembe mahali tutashukuru akitufikishia ili zifanyiwe kazi, lakini tujiepushe na taarifa za uzushi na uwongo zenye malengo ya kuchafua watu wengine kwa nia binafsi,” amesema Misime.


Awali katika taarifa yake, Mwanaharakati Malisa amebainisha kuwa Beatrice na Paul (Lucas) walikua kwenye mahusiano lakini Paul akawa anamtesa kwa vipigo vya mara kwa mara.


“Amewahi kumpiga mpaka mimba ikatoka. Beatrice alitafuta suluhu kwa muda mrefu bila mafanikio. Hatimaye akaamua kuondoka na kwenda kuanza maisha yake.


Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime


“Kabla ya kuondoka Tarimo alimpora kiasi cha Sh 10 milioni ambazo zilikua mtaji wa biashara pamoja na pesa za ujenzi wa nyumba ya mama yake. Beatrice aliripoti polisi lakini Tarimo hakuwahi kuitwa kuhojiwa.


“Beatrice alipoondoka kwa Tarimo aliacha baadhi ya mali ikiwemo nguruwe wakubwa sita na vitoto 11. Baada ya Beatrice kuondoka Tarimo alienda kwenye banda na kukatakata nguruwe wote pamoja na vitoto. Bado polisi hawakufanya lolote.


“Tarehe 13/11/2023 saa 12 jioni Beatrice akiwa na akina mama wengine wawili, walishambuliwa na Tarimo, ambaye alimkwida Beatrice na kumchoma jumla ya visu 25 maeneo mbalimbali ya mwili wake.


“Alikimbizwa hospitali ya Huruma lakini alipewa rufaa kwenda KCMC. Tayari ameshafanyiwa operation kubwa mbili za tumbo, na ameshonwa jumla ya majeraha ya nje zaidi ya 20. Kwa sasa yupo ICU. Yupo kwenye mstari mwembamba kati ya kifo na uzima. Wakati huohuo Tarimo anaendelea na shughuli zake kama vile hakuna kilichotokea,” Malisa aliandika.


Aliendelea kuandika kwamba, Beatrice ana watoto wawili ambao aliwazaa kabla hajakutana na Tarimo.


“Mmoja yupo chuo kikuu UDSM mwaka wa tatu na mwingine yupo darasa la tano. Katika hali ya kushangaza Tarimo amesema atawasaka watoto hao na kuwaua. Watoto hao wameripoti kutishiwa maisha kwenye kituo cha polisi Tarakea lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa,” aliandika Malisa katika ukurasa wake na kuomba vyombo vya dola ikiwamo IGP Camilius Wambura kuchukua hatua.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad