Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limemteua Mwenyekiti wa Shirikisho cha Klabu Afrika (ACA) na Rais wa Yanga, Hersi Saidi kuwa mjumbe wa Kamati ya Maandalizi za Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa ndani (Chan).
Hilo limesemwa leo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia katika mkutano mkuu wa mwaka wa shirikisho hilo unaoendelea mjini Iringa.
Karia amesema kuwa Hersi ameteuliwa kuingia katika kamati hiyo kwa vile ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF nafasi aliyoipata baada ya kuukwaa uongozi wa ACA.
"Kwa nafasi ya kuwa rais wa klabu Afrika, Hersi Said ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na hivyo ameingia kwenye Kamati ya Maandalizi ya Chan na Afcon," alisema Karia.
Hersi aliingia madarakani Yanga akirithi mikoba ya Dk Mshindo Msolla, ambapo katika uongozi wake amefanikiwa kuibadilisha timu hiyo kucheza soka la kisasa huku ikifanikiwa kusajili wachezaji wenye viwango vya juu Afrika.
Timu hiyo ambayo msimu huu imefanikiwa kupenya na kuingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita ilifanikiwa kufika fainali za Kombe la Shirikisho barani humu na kushindwa na USM Algier katika mchezo wa fainali.