KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza, ameshindwa kujizuia na kujikuta akimmwagia sifa kiungo fundi wa Yanga, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa soka tamu alilolipiga juzi kwenye pambano la Ligi Kuu kati ya Vijana wa Jangwani na Mtibwa Sugar akiziba kwa ufasaha pengo la Khalid Aucho aliyesimamishwa mechi tatu.
Mashabiki na mabosi wa Yanga walikuwa na presha kutokana na Aucho kutumikia adhabu na kuhisi labda timu hiyo ingeyumba eneo la kiungo cha ukabaji, lakini kocha Miguel Gamondi aliamua kumuanzisha Sure Boy juzi na kiungo huyo mkongwe hakumuangusha kwa kucheza kwa kiwango kilichowaibua wadau akiwamo Saido.
Aucho amefungiwa michezo mitatu na kupigwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumpiga kiwiko nahodha na kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu kwenye mchezo uliochezwa Novemba 8 mwaka huu na mchezo wa jana ulikuwa wa kwanza kuanza kutumikia adhabu hiyo.
Aucho alikosekana kwenye mchezo huo ambao Yanga ilishinda mabao 4-1, huku pengo la kiungo huyo likizibwa kiufundi na Sure Boy ambaye amewaibua mastaa mbalimbali ambao wamevutiwa na kiwango chake, akiwamo Saido aliyemsifia kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii.
Saido mwenye mabao matatu kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, aliandika kwenye ukurasa wake; Fundi mwenye ufundi wake, akiambatanisha na picha ya Sure Boy, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayekipiga kwa sasa Azam FC aliandika; kiungo wa mpira ‘Babu Kaju’ ulicheza vizuri jana,’ akisifia kiwango cha mkongwe huyo.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa Pyramids ya Misri, Fiston Mayele pia alimpongeza Sure Boy akiungana na mastaa wengine wa Yanga akiwamo Aucho aliyempongeza pia na kuweka wazi kuwa alikuwa na mchezo mzuri juzi.
Nyota wengine wa Yanga walimmwagia kifyagio Sure Boy ni pamoja na Pacome Zouzoua, Keneddy Musonda, Nickson Kibabage, kipa Metacha Mnata, Farid Mussa, Mudathir Yahya, Stephane Aziz Ki, Denis Nkane sambamba kiungo mkongwe wa zamani wa Simba na Azam, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
Kilichofanya mastaa hao kuungana kummwagia sifa Sure Boy asiye na nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Gamondi ni namna alivyokuwa akikaba, kutoa pasi na kutengeneza mashambulizi ya Yanga, huku akiituliza timu kwa muda mrefu.