Sakata la Gekul lachukua sura mpya


Sakata la Gekul lachukua sura mpya

Dar es Salaam. Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul ameitwa mahakamani, kujibu tuhuma za kumshambulia na kumdhuru Hashim Ally, Novemba 11, mwaka huu, kinyume na kifungu cha 241 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 ya mwaka 2022.

Wito huo uliotolewa leo Jumatatu, Desemba 11, 2023 na Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara baada ya wakili Peter Madeleka kumfungulia kesi ya jinai Novemba 11, mwaka huu.

Kulingana na barua ya wito huo (Mwananchi tumeiona), iliyogongwa muhuri wa mahakama hiyo, Gekul anapaswa kuripoti mahakamani hapo Desemba 27, mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo ikitajwa.

Katika wito huo, mlalamikaji ni Hashim Ally dhidi ya Pauline Gekul.


Akizungumzia wito huo, wakili wa mlalamikaji, Madeleka amesema umekuja baada ya kufungua kesi ya jinai ya shambulio la kudhuru mwili. "Kwa wito huo kesi itaanza kusikilizwa Desemba 27."

Alipotafutwa kuthibitisha iwapo amepokea wito huo, Gekul amesema hakuona wala kuupokea.

"Sijaona, sijapokea wala sifahamu chochote kuhusu hilo," amesema Gekul ambaye Novemba 25 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wake wa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria


Gekul anapokea wito huo, kipindi ambacho Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limewasilisha jadala la tuhuma zake katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi.

Mzizi wa yote hayo ni tuhuma zilizoibuliwa na Hashim Ally, zilizosambaa mitandaoni akiomba msaada kwa watetezi wa haki za binadamu ili apate haki yake baada ya kufanyiwa ukatili na mbunge huyo.

Katika kipande hicho cha video, Ally alieleza ukatili aliofanyiwa unatokana na kile kilichodaiwa kuwa ameshiriki kuweka dawa za kishirikina katika eneo la kazi na sumu kwenye chakula.

Kijana huyo alieleza baada ya kukana hayo, mbunge huyo alimtaka avue nguo na kuingizwa chupa kwenye makalio.


Mbali na hilo, kijana huyo alieleza pia alitishiwa bastola na kupelekwa polisi.

Tayari Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetaka uchunguzi wa kina ufanyike juu ya tuhuma za mbunge wake na akithibitika kuhusika achukuliwe hatua za kisheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad