ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza, amelia na kitendo cha mmomonyoko wa maadili kuongezeka kwenye jamii, hali aliyotaja kupelekea hofu ya Mungu kupungua na dhambi kubugiwa kama chakula. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kupitia salamu zake za siku kuu ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu, Noel maarufu kama Christmas, alizotoa kwa waumini wa dayosisi yake tarehe 14 Disemba 2023, Askofu Bagonza amedai kutokana na mmomonyoko wa maadili dhulma inashabikiwa wakati haki ikijeliwa.
“Wasema kweli ni maadui wa taifa na matapeli wanaitwa wazalendo na kuenziwa kama mashujaa. Haya yote yanatokea wakati hekalu liko kimya, sasa waliotakiwa kukemewa na kuonywa juu ya dhambi hizi ndiyo wanalikemea na kulionya kanisa,”
“Hekalu limezama na kujificha katika ibada, mikesha, sakramenti na kujenga mahekalu zaidi ambayo yamegeuka kuwa vitalu vya kuotesha na kustawisha ufisadi, dhulma na dhambi zote,” imesema taarifa ya Askofu Bagonza.
Kuhusu vitendo vya rushwa, Askofu Bagonza amedai kiwango chake kinawakatisha tamaa wapambanaji, badala ya kuungana kupambana na rushwa watu wanapambana na wanaopambana na rushwa.
“Hata wananchi wanyonge nao wanadai rushwa toka kwa viongozi wao waliowachagua. Hivi sasa dhambi si kutoa, kupokea wala kudai rushwa tu hata kujua, kushuhudia na kukaa kimya dhidi ya rushwa ni rushwa pia. Kimya cha viongozi kuhusu tatizo hili kina madhara makubwa kwa jamii,” imesema taarifa hiyo.
Kiongozi huyo wa kiroho amedai chanzo cha matatizo yote hayo ni miundombinu ya kidemokrasia kutowezesha viuongozi kuwajibika kwa Mungu na kwa wananchi.
“Tunahitaji mfumo mpya wa kidemokrasia unaowezesha viongozi kuogopa hukumu ya wananchi na hukumu ya Mungu. Dini zimezama katika wajasiriamali wa kirogo, dhambi za mfumo hazikemewi na dhambi binafsi ni mtaji wa viongozi wa dini kujinufaisha binafsi. Tunaalikwa kumlaki Yesu mkombozi wa roho, mwili na akili,” imesema taarifa hiyo.
Akizungumzia kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Askofu Bagonza amesema ni tumaini pekee la mabadiliko ya roho ambapo anawaalika waamini kuingia kwenye mchakato wa mabadiliko ya kweli.