Dar es Salaam. Kumeguka sehemu ya Mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyoya maji ya mvua, hivyo kuporomoka na kutengeneza tope ndicho chanzo cha maporomoko yaliyosababisha vifo vya watu 65 na kujeruhi wengine 117.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali Desemba 5, 2023 mgandamizo uliokuwapo mlimani ulisababisha sehemu iliyoshidwa kuhimili kumeguka na kuporomoka.
Maafa hayo yalitokea Jumapili alfajiri Desemba 3, 2023 kwenye mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta, pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.
Vitongoji vingine ni Arukushay na Sebasi, wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Kabla ya maporomoko hayo, mvua kubwa ilinyesha Jumamosi Desemba 2 kuanzia saa tatu usiku.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi katika taarifa kwa umma, amesema tope liliporomoka kwa kufuata mkondo wa mto Jorodom, likizoa mawe na miti na kwenda kupiga makazi ya binadamu yaliyokuwa pembezoni mwa mto.
“Mlima Hanang umeundwa na miamba laini ijulikanayo ‘volcanic sediments’ (chembechembe za mchanga uliotokana na kivolkano),” amesema na kuongeza:
“Serikali imefuatilia taarifa za matetemeko kuanzia Septemba 2023 hadi siku ya tukio na hakukuwa na tetemeko lolote wala mlipuko wa volkano. Uchunguzi ulifanywa kwa kupita kwa miguu, helikopta ili kufanya uchunguzi huo.”
Matinyi ameainisha mipango inayotekelezwa na Serikali ili kuwaisaidia waathirika wa maafa hayo.
Amesema kambi tatu zimewekwa katika shule tatu za kuwasaidia ikiwamo kuwapatia chakula, matibabu na malazi.
Mipango mingine amesema ni kuandaa na kugharimia mazishi ya watu wote waliopoteza maisha.
Amesema hadi leo Jumanne Desemba 5, 2023 maiti 60 zilichukuliwa na ndugu kwa ajili ya maziko huku tano bado hazijatambuliwa.
Mipango mingine amesema ni kutoa matibabu ya bure kwa waathirika wote, kuwapatia chakula na malazi ya dharura manusura waliopoteza makazi yao na majeruhi waliotoka hospitali.
Pia, kuondoa tope lililojaa mitaani na barabarani katika mji mdogo wa Katesh, kazi iliyoanza siku ya tukio na kuwezesha barabara kuu ya kutoka Babati kwenda Singida kufunguka.
Matinyi amesema mipango mingine ni kufukua mali na nyumba zilizozama kwenye tope na kutafuta iwapo bado kuna miili.
Amesema wamejipanga kurejesha huduma za umeme, maji, mawasiliano na kudhibiti usalama.
Pia kuondoa wananchi wengine ambao nyumba zao zimeathirika na waliopo kwenye njia ya maji kutoka milimani ili kuwaepusha na lolote linaloweza kutokea kwa siku zijazo.
Majeruhi
Matinyi amesema jumla ya majeruhi 117 walipokewa katika Kituo cha Afya Gendabi, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.
Kati yao, amesema majeruhi 18 hawakuwa katika hali nzuri ambao walihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa matibabu zaidi na mmoja alifariki dunia siku moja baadaye, Desemba 4, 2023 saa nne usiku.
Amesema majeruhi 17 bado wanaendelea na matibabu hospitalini hapo, huku wengine 74 wanatibiwa katika hospitali za Tumaini na Kituo cha Afya Gendabi, huku 25 walitibiwa na kuruhusiwa.
Waathirika
Matinyi amesema hadi sasa kuna waathirika 190 waliohifadhiwa katika shule za Katesh, Gendabi na Ganana. Hata hivyo, amesema walioko Shule ya Msingi Ganana watahamishiwa katika shule ya Sekondari ya Katesh kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa huduma.
Madhara kwa ujumla
Amesema kaya 1,150 zenye watu 5,600 zimepoteza makazi katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi.
Msaada
Matinyi ametoa wito kwa kampuni, mashirika, taasisi za umma na binafsi, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitolea kwa hali na mali kuwasaidia waathirika wa tukio.
Amesema bado msaada unahitajika ukiwamo wa vyakula, mitambo na dawa.
“Kwa misaada ya fedha, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ameelekeza kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022, fedha zote zitumwe kwenye akaunti ya Kamati ya Maafa ya Taifa namba 9921151001,” amesema Matinyi.