Simba: Kutajwa FIFA ni heshima kubwa, tutapambana

 

Simba: Kutajwa FIFA ni heshima kubwa, tutapambana

Klabu ya Simba SC imeweka wazi kuwa, timu yao itajipanga vyema kuvuna alama za kutosha katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24, ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano mipya ya Kombe la Dunia kwa klabu itakayotimua vumbi Juni 15 hadi Julai 13, 2025.


Simba SC ni miongoni mwa timu 12 kutoka Afrika zenye nafasi kubwa ya kushiriki michuano hiyo kufuatia alama itakazovuna katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.


Iko hivi, Simba SC inayoshika nafasi ya saba ikiwa na alama 45 katika viwango vya ubora Afrika, ili ifuzu kucheza Kombe la Dunia inapaswa kuvuna alama nyingi kuizidi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyopo nafasi ya tatu kwa alama 81 au itwae ubingwa wa Afrika msimu huu.


Michuano mipya ya Kombe la Dunia kwa klabu itashirikisha timu 31 kutoka mashirikisho sita ya soka duniani, wakati Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitarajiwa kutoa klabu nne.


Katika mchanganuo wa klabu hizo, Al Ahly ya Misri iliyotwaa ubingwa wa Afrika msimu uliopita na Wydad AC ya Morocco iliyobeba msimu wa 2021 /22, tayari zimeshajihakikishia nafasi ya kushiriki michuano hiyo, huku timu mbili nyingine zitakazoshiriki zitakuwa ni bingwa wa msimu huu na timu itakayokuwa na pointi nyingi.


Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo ndiyo muandaaji wa michuano hiyo, Kombe la Dunia kwa klabu litafanyika kwa mfumo wa makundi na baadae kwenda hatua ya mtoano huku ikiwa haina mshindi wa tatu.


Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema timu yao kutajwa kuwania nafasi hiyo ni heshimna kubwa na Wanasimba wa wanapaswa kujivunia.


Pia, amesema uongozi wa klabu utaijenga vyema timu kwa kushirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha wanafikisha pointi za kutosha kushiriki michuano hiyo.


“Timu yetu kutajwa tu ni jambo la kujivunia, sisi kama viongozi tutahakikisha tunapambana kuijenga timu kuendelea kufanya vizuri hasa katika mashindano ya kimataifa tuweze kuwa bora zaidi na kuipeperusha vyema bendera ya nchi,” amesema.


Timu zingine zilizopo katika orodha ya miamba 12 bora ya viwango vya CAF ni ES Tunis ya Tunisia ikiwa nafasi ya nne kwa alama 75, CR Belouizdad ya Algeria nafasi ya tano kwa alama 59, Petro de Luanda ya Angola ikiwa katika nafasi ya sita kwa alama 49.


Raja Casablanca ya Morocco inashika nafasi ya nane ikiwa na alama 45, Al Hilal ya Sudan ina alama 33 katika nafasi ya tisa, Horoya ya Guinea nafasi ya 10 kwa alama 29, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini nafasi ya 11 kwa alama 28 sawa na Zamalek ya Misri ikiwa nafasi ya 12.


Pamoja na Simba SC kuwa na nafasi kubwa, kikosi cha Young Africans nacho kinavweza kufuzu kucheza michuano hiyo ikiwa kitatwaa ubingwa wa Afrika msimu huu 2023/24.


Youn g Africans ipo Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikiwa na timu za Al Ahly, CR Belouizdad na Medeama ya Ghana.


Katika kundi hilo, Young Africans inashika nafasi ya pili kwa alama tano baada ya kushuka dimbani mara nne, kinara Ahly ina alama tano, CR Belouizdad nafasi ya tatu kwa alama nne sawa na Medeama SC ya Ghana iliyopo nafasi ya nne.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad