YANGA inashuka jioni ya leo kwenye Uwanja wa Azam Complex katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini wakimaliza watarudi kibaruani katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuialika Medeama, huku mashabiki 45,000 wakipata mchekea baada ya tajiri kuwapa jeuri.
Tajiri wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ amenunua tiketi zote za mzunguko kwenye pambano hilo la marudiano ya Kundi D litakalopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya mechi ya awali iliyopigwa wikiendi iliyopita kumalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Kumasi, Ghana.
Yanga inahitaji ushindi ili kujiweka pazuri kwenye kundi linaloongozwa na mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri wanaofuatiwa na Medeama kisha CR Belouizdad ya Algeria. Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, tajiri huyo ameamua kuwavuta mashabiki uwanjani kwa kununua tiketi zote za mzungumo ambazo zitapewa mashabiki zikiwa na thamani ya Sh135 milioni kwani kiingilio ni Sh3,000 kwa kichwa. Yanga kama ikitinga robo fainali itaji-hakikishia kiasi cha Dola 900,000 (takriban Sh2.2 bilioni).