Siku moja baada ya Bunge la Umoja wa Ulaya kulaani kuhamishwa jamii za watu wanaoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro, serikali ya Tanzania imetoa wito kwa Bunge hilo kwenda kukagua eneo hilo.
Katika taarifa iliyotolewa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi inaeleza kuwa Tanzania inalikaribisha Bunge la Ulaya kwani “serikali haina kitu cha kuficha na inahakikisha wakati wote haki za binadamu zinaheshimiwa.”
Kwa upande mwingine, Matinyi ameweka wazi kuwa Serikali ya Tanzania inatambua kwamba shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi elimu na utamaduni (UNESCO), litapeleka wataalamu wake mwezi Januari 2024 kufanya ukaguzi.
Tanzania imeendelea kukanusha madai ya kuhamishwa jamii hizo kwa nguvu, ikisisitiza kuwa wanahama kwa hiari kwenda katika maeneo ambayo serikali imewajengea miundombinu yote muhimu.
Msemaji wa serikali aliongeza kuwa Tanzania haikaliwi kutokana na makabila ya watu.
"Eneo la Ngorongoro lina makabila zaidi ya moja na Serikali haitambui watu wake kwa makabila na kila mtu wa kabila lolote nchini ana haki ya kuishi popote nchini. Kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu hakuna kabila au kundi la watu lenye hadhi ya “watu wa asili” (indigenous peopl