Trafiki Watakiwa Kuzidisha Tochi Kuzuia Ajali barabarani Kisa Ajali


Ajali ya Basi
Ajali ya Basi

Trafiki watakiwa kuzidisha tochi kuzuia ajali barabarani
Mwanza. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amelitaka Jeshi la Polisi nchini kitengo cha usalama barabarani kuzidisha tochi ili kudhibiti ajali za barabarani zinazoonekana kushika kasi hivi karibuni.

Novemba 26, mwaka huu ilitokea ajali ya basi la Kampuni ya Baraka lililokuwa likitokea Tandahimba, mkoani Mtwara kuelekea Dar es Salaam iliyoua watu 15 na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.

Ajali nyingine ilitokea Novemba 29, 2023 ikiua watu 13 na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Ally's Star lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kugonga treni ya mizigo katika makutano ya barabara na reli maeneo ya Manyoni mkoani Singida.

Akitoa maagizo hayo Desemba Mosi, 2023 wakati akifunga semina ya usalama barabarani kwa Ukanda wa Afrika iliyohusisha nchi zaidi ya 27 kutoka Afrika na Ulaya, Kihenzile amesema ni bora Trafiki walaumiwe kuzidisha tochi kuliko nchi kuendelea kupoteza Watanzania kwenye ajali zinazoweza kuzuilika.


“Ninyi ni mashahidi na mnafahamu kila siku tunasikia ajali watu wanakufa, watu wanavunjika, vyombo vinaharibika athari kubwa kwenye nchi tunapata na sio kwenye nchi yetu tu na hata nchi zingine.

“Niwaombe wenzangu wa vyombo vya usalama ongezeni kusimamia sheria. Ni mara 1,000 mlaumiwe mmezidisha tochi kuliko taifa kuendelea kushuhudia vifo vya wasio na hatia, nguvu kazi, wazazi wanazidi kufariki wanawaacha watoto. Kwahiyo nawaagiza hasa kipindi hiki cha sikukuu lazima wenzetu mzingatie kusimamia vikali. Watawalaumu lakini mara 1,000 wawalaumu ili muokoe maisha ya wasio na hatia,”amesema

Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Road Safety Initiatives (TARSI) linalojihusisha na utoaji elimu ya usalama barabarani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema jeshi hilo limepokea maelekezo akiahidi litaongeza ukali kwa wote watakaoshindwa kufuata sheria za usalama barabarani.


Mkurugenzi wa TARSI, Mariki Barongo amesema semina hiyo ya siku tano imewanoa washiriki kuanzia kwenye ujenzi wa barabara hadi usimamizi wa sheria za barabarani ambapo wadau mbalimbali wakiwemo kutoka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijinini (Tarura) na Jeshi la Polisi kitendo cha Usalama Barabarani walishiriki.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad